Habari MsetoSiasa

Hakuna atakayesazwa katika vita dhidi ya ufisadi – PAC

July 11th, 2018 2 min read

?Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) imepuuzilia mbali madai ya magavana kwamba vita vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelea vinalenga serikali za kaunti pekee huku serikali kuu ikisazwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo James Opiyo Wandayi Jumanne alisisitiza kuwa vita hivyo vinavyoongozwa kwa pamoja na asasi mbalimbali za serikali zilianzia katika ngazi ya serikali kabla ya kuendelezwa katika serikali za kaunti.

“Ningependa kuwafahamisha magavana kwamba hakuna yoyote atakayesazwa katika vita hivi. Maafisa kadhaa wa serikali kuu wameandamwa.

Mifano ni kama vile Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia, aliyesimamishwa kazi na kushtakiwa Bi Lilian Omollo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Vijana kwa Huduma ya Taifa (NYS) Richard Ndubai na Mkurugenzi wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs),” akasema Bw Wandayi ambaye pia ni mbunge wa Ugunja.

Mbunge huyo alikuwa akijibu madai yaliyotolewa na mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Josephat Nanok aliyedai kuwa serikali inalenga wakuu wa kaunti pekee katika vita vinavyoendelea dhidi ya zimwi la ufisadi.

“Inaonekana wazi kwamba vita hivi vya ufisadi vinawalenga magavana pekee huku maafisa wa serikali kuu wakisazwa. Hii ni kwa sababu baada ya kukamatwa kwa Mheshimiwa Ojaamong'(Gavana wa Busia) sasa tunasikia wenzetu wengine watakamatwa katika wiki zijazo,” akasema Bw Nanok ambaye ni Gavana wa Turkana.

Gavana huyo ambaye alikuwa ameandamana na Bw Ojaamong, Paul Chepkwony (Kericho) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) alilalamikia kile alichosema ni kudhalilishwa kwa Gavana huyo wa Busia ambaye ameshtakiwa kwa tuhuma za kutoa zabuni ya kima cha Sh8 milioni.

Bw Ojaamong alikamatwa Jumanne wiki jana alipojiwasilisha katika makao makuu ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kupendekeza kuagiza afunguliwe mashtaka.

Bw Wandayi aliwaambia magavana kukubali kuwajibishwa kutokana na hitilafu za kifedha katika kaunti zao, kwa sababu wao ndio wakuu wa kaunti hizo.

“Magavana sharti wawajibike. Hawafai kulalamika huku wakimtetea mwenzao ambaye anakabiliwa na kesi mahakama. Nanok na wenzake watulie kwani bila shake Bw Ojaamong ataachiliwa huru ikiwa mahakama itabaini kuwa hana makosa,” akasema.