‘Hakuna kifo cha corona jana Jumatano’

‘Hakuna kifo cha corona jana Jumatano’

Na CHARLES WASONGA

KENYA Jumatano, haikuandikisha kisa chochote cha maafa kutokana na ugonjwa wa Covid-19 huku visa 485 vipya vya maambukizi vikithibitishwa ndani ya muda wa saa 24.

Hii ina maana kuwa idadi jumla ya watu waliofariki kutokana na maradhi hayo inasalia 3,428.

Visa hivyo vipya sasa vimefikisha idadi jumla ya visa hivyo nchini kuwa 176,622 tangu Machi 13, 2020 kisa cha kwanza kilipogunduliwa nchini.

Watu hao 485 wamepatikana na virusi vya corona baada ya sampuli 5,355 kupimwa ndani ya muda wa saa 24

Kulingana na taarifa iliyotumwa na Wizara ya Afya kwa vyombo vya habari, idadi ya watu waliopona corona ilipanda hadi 121,206 baada ya watu 312 zaidi kuthibitishwa kupona.

“Miongoni mwa waliopona 219 walikuwa wakiuguzwa nyumbani ilhali 93 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Jumla ya wagonjwa 1,076 wa Covid-19 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini wa huku jumla ya wagonjwa 4,810 wakihudumiwa chini ya Mpango wa Uuguzi Nyumbani.

Vile vile, jumla ya wagonjwa 102 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICUs), 29 kati yao wakiwa wamewekwa katika mitambo ya kuwasaidia kupumua huku 60 wakiongezewa hewa ya oksijeni.

Wakati huo huo, kaunti za Nyanza na Magharibi mwa Kenya zinaendelea kuandikisha visa vingi vya maambukizi japo Nairobi inaongoza kwa visa vipya vilivyothibitishwa Jumatano.

Nairobi ina visa 119, Homa Bay ina visa vipya 68, Siaya (61), Kisumu (48), Mombasa (28), Busia (24), Kakamega (19), Kericho (16), Nakuru (14), Bomet (13), Uasin Gishu (11), Bungoma (10) na Vihiga imeandikisha visa vinane.

Kaunti za Kisii na Machakos nazo zimenakili visa saba kila moja, Kilifi (5), Nyeri (4) na Narok (4) Migori (3), Kajiado, Kiambu, Kirinyaga, Kitui, Nyandarua Pokot Magharibi zina visa viwili kila moja huku Kwale, Laikipia, Murang’a na Nyamira zikirekodi kisa kimoja kila moja.

You can share this post!

Msipoungana msahau urais milele, Ngilu aambia vinara wa Nasa

Mabeki Maguire na Tierney kurejea katika vikosi vyao vya...