Habari MsetoSiasa

Hakuna Krismasi, Kimemia aambia wafanyakazi wake

December 20th, 2018 1 min read

Na WAIKWA MAINA

WAFANYAKAZI wa serikali ya kaunti ya Nyandarua hawatapumzika kwa sherehe za Krismasi, huku hata waliokuwa likizoni wakiamrishwa kurejea kazini na Gavana Francis Kimemia. Wahudumu hao wanahitajika kukamilisha miradi mingi ambayo imekwama tangu mwaka uliopita.

Gavana Kimemia alitoa amri hiyo Jumanne baada ya mkutano wa siku nzima na maafisa wakuu wa kaunti kukagua namna idara tofauti za serikali hiyo zilifanya kazi mwaka uliopita.

Ilibainika kuwa miradi mingi ya kipindi hicho haikukamilika. Hivyo basi, iliamuliwa sharti ikamilishwe pamoja na ile iliyopangwa kutekelezwa katika kipindi cha kifedha cha 2018/2019.

Baadhi ya miradi iliyoathirika zaidi ni ya ujenzi wa barabara ambayo ilikosa kukamilika kutokana na msimu wa mvua ambao ulivuruga kazi.

Mwaka huu, ujenzi wa barabara katika kaunti hiyo umetengewa Sh1.1bilioni ambazo gavana huyo alisema sharti zikamilike kabla ya msimu wa mvua kuanza tena.

“Ni wafanyakazi wanaotakiwa kutekeleza, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi hii, wakienda likizoni ni nani atahakikisha kazi imefanywa. Kutoa huduma ndilo lengo kuu la serikali. “kwa hivyo, hakuna mfanyakazi ataondoka kazini na wale wako likizoni warejee mara moja,” aliamuru.