Habari

HAKUNA KUPUMUA: Gharama ya maisha kuzidi kupanda

July 19th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

GHARAMA ya maisha inatarajiwa kupanda zaidi kuanzia katika muda siku 10 zijazo kutokana na ushuru mpya wa bidhaa. Kodi hii ni kando na iliyowekwa kwenye bajeti mwezi uliopita.

Ushuru huu mpya unahusu bidhaa kama maji, sharubati, pikipiki na marupurupu ya wafanyakazi. Wanywaji pombe pia wataumia kwani vileo pia vitapanda bei.

Hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi mwezi Septemba wakati bidhaa za mafuta zitakapoanza kutozwa ushuru mpya wa ziada (VAT). Hii ni kutokana na kuwa ongezeko la bei za mafuta husababisha kupanda kwa bei za bidhaa za kimsingi kutokana na gharama za usafirishaji bidhaa.

Kwa sasa, bei ya petroli ni Sh113 kwa lita jijini Nairobi na viunga vyake na inatazamiwa kuongezeka hadi Sh130 kuanzia Septemba. Hii inamaanisha kuwa bei za unga, sukari, usafiri miongoni mwa zingine pia zitapanda wauzaji wakipitisha gharama kwa wanunuzi.

Kulingana na kampuni ya PricewaterhouseCoopers (PwC), KRA haikuongeza kodi ya bidhaa za mafuta kwenye bajeti ya Juni kwa sababu ya ushuru mpya wa VAT kwa bidhaa za mafuta utakaonza kutumika Septemba.

Kwenye mwongozo wa ushuru ambao KRA ilichapisha Ijumaa wiki jana, Wakenya watakuwa wakitozwa ushuru mpya wa moja kwa moja wanaponunua maji ya chupa, sharubati na mjazo wa simu kuanzia Agosti.

Kwa mara ya kwanza, KRA itaanza kutoza ushuru mpya wa asilimia 5.2 kwa bidhaa hizi jambo ambalo shirika hilo linasema ni kuepusha serikali na athari za kupanda kwa gharama ya maisha.

Katika mwongozo huo mpya, ushuru wa lita moja ya sharubati ya matunda utaongezeka kutoka Sh10 hadi Sh10.5 nao wa maji utapanda kutoka Sh5 hadi Sh5.2 kwa lita. Watengenezaji wa bidhaa hizi watapitisha gharama hiyo kwa wateja kwa kupandisha bei.

Wanaopenda starehe pia watalazimika kujikaza huku bei ya pombe ikitarajiwa kuongezeka baada ya watengenezaji kutozwa ushuru mpya wa Sh105.2 kwa lita kutoka Sh100 kwa lita.

Sekta ya uchukuzi nayo itaathiriwa baada ya ushuru unaotozwa pikipiki maarufu kama bodaboda kupanda kutoka Sh10,000 hadi Sh10,520.

Kwenye bajeti ya mwaka huu, serikali ilisema ingeongeza kiwango chake kwa ukusanyaji ushuru kwa kutoza watengenezaji wa bidhaa za kimsingi ushuru wa thamani ya ziada (VAT). Hii inamaanisha nao watapitisha gharama hiyo kwa watumiaji bidhaa hizo. Hatua hii itafanya bei ya unga kupanda kutoka wastani wa Sh100 kwa sasa hadi takriban Sh120 kwa paketi moja ya kilo mbili.

Bei za mkate na maziwa pia zitapanda kutoka wastani wa Sh50 hadi zaidi ya Sh60.

Waziri Rotich pia alipandisha ushuru unaotozwa mafuta taa na kuuweka kiwango sawa na ule unaotozwa petroli na gesi ya kupikia, akisema hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi ya mafuta taa.

Kulingana na KRA, kuanzia Agosti ushuru wa bidhaa kama pombe, sigara, maji ya chupa na sharubati utakuwa ukiongezeka kila mwaka kwa kutegemea kupanda kwa gharama ya maisha.

Hii inamaanisha kuwa kila mwaka gharama ya maisha ikipanda, ndivyo Wakenya watakuwa wakiendelea kuumia.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba lengo la serikali ni kuiepusha na athari za mfumko wa gharama ya maisha.

KRA pia inalenga kutoza ushuru marupurupu ya wafanyakazi kutoka kwa waajiri wao.

kama vile ya kununua magari, chakula na mjazo wa simu. Tayari ushuru wa kutuma pesa kwa simu umeongezeka kutoka asilimia 10 hadi 12.

Kuanzia sasa watakuwa wakitozwa ushuru wa asilimia 12.7 kwa kutuma pesa kwa simu. Katika mswada wa fedha wa 2018, Bw Rotich alipendekeza awe akibadilisha ushuru kila mwaka tofauti na awali mabadiliko yalipofanywa baada ya miaka miwili.