Habari

Hakuna kupumua shuleni

November 17th, 2020 2 min read

MARY WANGARI na VALENTINE OBARA

WANAFUNZI wa shule za msingi na upili wanatazamiwa kukumbana na masomo ya kuharakishwa watakaporudi shuleni hapo Januari.

Katika juhudi za kurekebisha kalenda ya elimu iliyovurugwa na janga la corona, Wizara ya Elimu, Jumatatu ilitoa ratiba mpya itakayodumu hadi mwaka wa 2023.

Kwa mujibu wa kalenda hiyo, wanafunzi wote watarejea shuleni rasmi Januari 4, 2021 kwa muhula wa pili wa masomo hadi Machi 19, 2021.

Uchanganuzi wa kalenda hiyo umeonyesha kuwa, kuanzia mwaka ujao, likizo nyingi zitakuwa fupi mno kuliko kawaida.

Hatua hii itafanya muhula wa kwanza uwe ukianza katikati ya mwaka, hadi mwaka wa 2023 ambapo inatarajiwa mwaka wa masomo kurejelea hali ya kawaida kwa sababu utakuwa ukianza Januari.

Akizungumza Jumatatu alipotangaza ratiba hiyo, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alihakikishia wazazi kwamba serikali inajitahidi kikamilifu kuhakikisha watoto wote watakuwa salama wakiendeleza masomo yao.

“Tunajifunza mengi muhumu kutokana na jinsi shule zilivyofunguliwa kwa awamu tangu Oktoba. Tuna imani kwamba tutaendelea kupata suluhisho litakalohakikisha shule zetu ni salama kwa wanafunzi na walimu,” akasema Prof Magoha.

Mnamo Januari 4, 2021 wanafunzi wa PP1 na PP2, Gredi 1, 2 na 3, Darasa la 5, 6 na 7 na Kidato cha 1, 2 na cha 3 ambao wamekuwa nyumbani watahitajika kurudi shuleni.

Waziri alisema watoto wengine wote walio na umri wa miaka minne na zaidi watajiunga na PP1 Julai 2021.

Prof Magoha aliyekuwa akizungumza katika Taasisi ya Kuendeleza Mtaala Kenya (KICD) jijini Nairobi, alitoa tangazo hilo baada ya mkutano wa saa kadhaa na wadau mbalimbali katika sekta ya elimu.

Katika ratiba hiyo nzima, likizo ndefu itakuwa moja pekee, ya wiki saba, ambayo itadumu kuanzia Machi 20 hadi Mei 9, 2021.

Likizo hiyo imenuiwa kuruhusu watahiniwa wa mitihani ya kitaifa ya darasa la nane (KCPE) na kidato cha nne (KCSE) kukamilisha mitihani yao.

Likizo nyingine zilizobaki ni kati ya wiki moja hadi mbili.

Aidha, Bw Magoha alisema kuwa serikali itawapa barakoa wanafunzi kutoka jamii maskini, akitoa wito kwa wahisani kusaidia kutoa barakoa za kutumika shuleni.

Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC) lilitoa rasmi ratiba mpya ya mitihani ya KCPE na KCSE.

Mtihani wa KCSE ambao ungefanyika mwaka huu, sasa umepangiwa kuanza rasmi Machi 25 hadi Aprili 25, 2021. Hata hivyo, mitihani ya utenzi itaanza Januari.

Kwa upande mwingine, watahiniwa wa KCPE wamepangiwa kufanya mitihani yao kuanzia Machi 22 hadi Machi 24, 2021.

Hatua ya serikali ilijiri kufuatia amri ya Rais Uhuru Kenyatta mnamo November 12, 2020, alipoagiza Wizara ya Elimu kutoa mwelekeo kuhusu kurejelewa kwa masomo nchini kabla siku 14 zikamilike.

Wakati huo huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia, alisema walimu walio na umri wa miaka 58 kwenda juu na walio na matatizo ya kiafya wanapaswa kukaa nyumbani akiwahakikishia kuwa hawatafutwa kazi.

“Hii ni amri ya Afisi ya Rais, hamtafutwa kazi. TSC imeafikiana kuwalinda walimu dhidi ya maradhi yanayohusiana na Covid-19,” akasema.

Shule zilifungwa Machi wakati janga la corona lilipoingia nchini.

Wanafunzi wa Gredi Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne waliagizwa kurudi shuleni Oktoba 12.