Hakuna kura ya ugavana Mombasa, Kakamega leo

Hakuna kura ya ugavana Mombasa, Kakamega leo

NA WAANDISHI WETU

WAKAZI wa Kauti za Mombasa na Kakamega watalazimika kusubiri muda mrefu zaidi kabla kuchagua magavana wapya.

Hii ni baada ya karatasi za kura za nyadhifa hizo kukosekana hapo jana Jumatatu.

Maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Jumatatu walikuwa mbioni kurekebisha hali hii lakini baadaye, mwenyekiti, Bw Wafula Chebukati akasema imeamuliwa chaguzi hizo ziahirishwe hadi wakati mwingine utakaotangazwa baadaye.

Vilevile, Bw Chebukati alitangaza tume imeahirisha chaguzi za ubunge Kacheliba na Pokot Kusini.

Uchaguzi wa viongozi wengine katika maeneo hayo utaendelea ilivyopangiwa.

Wakati wa kufungua makasha ya karatasi za kura, ilibainika kuwa karatasi za ugavana zilizopokewa Mombasa zilikuwa ni za uchaguzi wa Kaunti ya Kilifi.

Makasha mawili yaliyofunguliwa katika kituo cha kujumuisha kura za eneobunge la Mvita kilicho Shule ya Upili ya Alidina Visram, yalibainika kuwa na vijitabu ambavyo vilinakiliwa kuwa vya uchaguzi wa ugavana Mombasa lakini ndani, karatasi zikawa na picha za wagombeaji ugavana wa Kilifi.

Taharuki ilitanda kwa muda huku maajenti wa wagombeaji ugavana wakitaka majibu kutoka kwa IEBC.

“Naomba tuwe watulivu. Bado kuna wakati wa kulirekebisha. Ni kosa dogo ambalo linaweza kufanyiwa marekebisho,” alisema Msimamizi wa Uchaguzi wa eneobunge la Mvita, Bw Sudi Masha.

Makasha yaliyofunguliwa katika kituo cha uchaguzi kilicho Shule ya Msingi ya Mikindani, eneobunge la Jomvu, na katika kituo cha eneobunge la Kisauni pia yalipatikana kuwa na karatasi za ugavana za Kilifi.

Mkuu wa uchaguzi wa eneobunge hilo, Bi Husna Hassan, alisema wakuu wa IEBC wangetoa taarifa baadaye kuhusu suala hilo.

Mkuu wa IEBC katika eneobunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi, Bi Aisha Abubakar, alithibitisha hawakuwa wamepokea karatasi za ugavana za kaunti hiyo asubuhi.

Hali sawa na hii ilishuhudiwa katika Kaunti za Kakamega na wadi ya Chuka/Igambang’ombe iliyo Kaunti ya Tharaka Nithi.

Katika Kaunti ya Kakamega, afisa mkuu wa uchaguzi, Bw Joseph Ayata, alithibitisha karatasi za kura za ugavana zilizopokewa zilistahili kuwa za Kaunti ya Kirinyaga.

Mkuu wa uchaguzi katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Bw Mohamed Raka, alithibitisha karatasi za uchaguzi wa udiwani za Fafi, Kaunti ya Garissa, zilikuwa zimepatikana Chuka/Igambang’ombe.

Vilevile, Bw Raka alisema karatasi za uchaguzi wa udiwani wa Wadi ya Mugwe, Kaunti ya Tharaka Nithi, zilikuwa zimepatikana Kaunti ya Garissa.

Akizungumza mjini Mombasa, mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea binadamu la Haki Africa, Bw Hussein Khalid, aliondolea lawama a IEBC akisema upakiaji hufanywa kule ng’ambo ambapo karatasi huchapishwa na hazifunguliwi hadi zifike hapa.

Katika Kaunti ya Lamu, IEBC jana ilianza kusafirisha vifaa vya kupigia kura na makarani hadi maeneo ya msitu wa Boni na maeneo yanayopakana na Somalia kwa kutumika helikopta.

Mkuu wa IEBC katika Kaunti ya Lamu, Bw Maro Ade, alisema tume hiyo ilikuwa tayari imefikisha helikopta ambayo itakuwa ikikaa mjini Faza ili kusambaza vifaa na wahudumu hadi maeneo yaliyo na changamoto za usafiri na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi.

Ripoti za Farhiya Hussein, Winnie Atieno, Alex Kalama, Brian Ocharo, Collins Omulo, Benson Amadala, Alex Njeru na Kalume Kazungu

  • Tags

You can share this post!

Gachagua, Karua wapiga kura Sagana na Mugumo mtawalia

Omar Shallo wa UDA akamatwa Mvita

T L