HabariMichezo

Hakuna Matata: Watanzania na Wakenya wazozana baada ya Dortmund kutumia Kiswahili Twitter

September 18th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA na Watanzania wanazidi kurushiana cheche za maneno baada ya timu inayocheza ligi ya Bundesliga, Borussia Dortmund, kuandika kwa lugha ya Kiswahili katika akaunti yake ya Twitter.

Timu hiyo ya Ujerumani ambayo iko katika nafasi ya pili kwenye jedwali la Bundesliga baada ya kucheza mechi nne, ilitia picha ya viatu katika mtandao wa Twitter na kisha kuandika: “Hakuna Matata”.

Watanzania na Wakenya waling’ang’ania umiliki wa maneno hayo pamoja na lugha ya Kiswahili.

‘Waafrika bado tuna shida, mbona Wakenya na Watanzania wanagombania Kiswahili? Lugha hii ni yetu sote,” akasema @sn_fahd katika juhudi za kupoza joto.

“Dortmund waje wakite kambi nchini Kenya wakutane na samba. Sinema yenyewe yaonyesha mandhari ya Hells Gate, katika nchi yetu tukufu,” akasema D’von Murimi.

Lakini @FredrickLeria alimjibu kwa haraka kwa kusema: “Hayo ni makosa, wacha waje Tanzania waone samba halisi katika mbuga za Serengeti na Ngorongoro na wapande Mlima Kilimanjaro.”

“Lugha ya Kiswahili ilianzia Mombasa Kenya wakati wa biashara ya watumwa. Someni historia,” akasema @amujkuntakinte.

Lakini Mtanzania @Kamigakikumbise akamjibu bila kupoteza wakati: “Kiswahili kilichoanzia Mombasa hakikuwa Kiswahili halisi, soma historia kwa umakini.”

Mtanzania mwingine @Chaza97_tz akadakia: “Usilete vizungu vingi Kiswahili kimetokea Tanzania.”

“Msidhani Watanzania ni wajinga kiasi hicho, la hasha. Sisi ni wastarabu hatupendi kujivuna kama Wakenya.. sio kwamba tumesinzia na hatuoni mambo mnayotufanyia huwa tunapuuza tu,” akasema @mwangiezeyy aliyoenekana kupandwa na jaziba.

Lakini Alexander Kabelindde alitoa ushauri kwa wapenzi wa Kiswahili:

“Ni jambo la aibu kuanza kukumbushwa juu ya lugha au utamaduni wako na watu wengine. Kama kweli ni lugha yako na unaipenda endelea hivyo hivyo. Kiswahili ni lugha yetu sote. Mnaoendeleza malumbano kuwa chanzo chake ni Tanzania na wengine Kenya, muwe mabalozi wazuri. Msipotoshe.”