Habari Mseto

Hakuna mikopo ya muda mfupi kwa serikali za kaunti – Ruto

November 12th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

BARAZA Shirikishi la Bajeti na Masuala ya Uchumi (IBEC) limetupilia mbali ombi la serikali za kaunti kutaka ziruhusiwe kuchukua mikopo ya muda mfupi (short-term loans) kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Akitoa tangazo hilo Jumatatu, Naibu Rais William Ruto alisema kuwa hatua hiyo ni kufuatia makubaliano baina ya mataifa ya Afrika Mashariki kuwa mataifa yake hayataweza kuchukua mikopo kutoka kwa benki kuu za nchi zao.

“Mataifa ya Afrika Mashariki yamekubaliana kuwa serikali hazitaweza tena kuchukua mikopo kutoka kwa benki kuu. Hatua hii inatarajiwa kuchukua mkondo kuanzia mwaka 2021,” akasema Dkt Ruto.

 

Naibu Rais William Ruto (kulia) akiwa na viongozi wengine Novemba 11, 2019, katika makao rasmi ya mtaani Karen. Picha/ Magdalene Wanja

Akaongeza: “Kutupiliwa mbali kwa ombi hilo ni kwa sababu serikali kuu iko katika hatua ya kujiondoa kutoka kwa uombaji fedha kutoka kwa benki kuu.”

Ruto alizungumza wakati wa mkutano na wanachama wa IBEC ambao ulihudhuriwa na magavana na wawakilishi kutoka kwa ofisi ya hazina na ile ya Ugavi wa Fedha za Kaunti yaani County Revenue Allocation.

Naibu Rais alisema kuwa Sh62 milioni za mgao wa serikali za kaunti tayari zimepeanwa huku akiongeza kuwa kaunti 20 tu ndizo hazijapokea mgao wao.

Aliongeza kuwa walikuwa wamebuni njia ambazo zitawezesha kaunti kujitegemea kifedha.

“Serikali za kaunti sasa zitaweza kupokea mkopo wa hadi asilimia 20 ya bajeti yao binafsi na ile ya mgao,” aliongeza.