Habari Mseto

Hakuna Mkenya ataangamia kwa njaa tena – Serikali

February 14th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

SERIKALI itaanza kutoa chakula cha msaada katika maeneo yanayoathiriwa na ukame kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanasalia shuleni.

Katika taarifa, serikali ilitangaza kuweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kuwa watoto wote wanaendelea na masomo bila kutatizwa na ukame na njaa.

Ilitangaza kuwa tayari kukabiliana na hali zozote za dharura zinazoweza kuletwa na ukame.

Mawaziri sita walikutana Jumatano na kujadiliana na kutathmini ripoti kuhusu hali ya ukame nchini kutoka kwa Mamlaka ya Kusimamia Hali ya Ukame (NDMA) na jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.

Ingawa kuna hali ya ukame, ikilinganishwa na mwaka uliopita, hali ya ukame sio mbaya sana kulingana na NDMA.

Kulingana na ripoti hiyo, kaunti 14 zinakabiliwa na hali ya kawaida ya ukame ilhali kaunti zingine tisa zimepewa tahadhari ilhali hali katika zingine 13 hali ya ukame inaendelea kudhoofika ambazo ni Garissa, Isiolo, Kitui, Marsabit, Samburu, Tana River, Turkana, Wajir, Kilifi, Laikipia, Mandera, Nyeri (Kieni area) na Pokot Magharibi.

Hatua zilizochukuliwa zinahusu afya, lishe, amani na usalama ambazo zinaweza kutatiza masomo hasa katika maeneo kame.

“Kutokana na hilo, utoaji wa dharura wa chakula, maji na bidhaa zingine zitatolewa katika nyumba, jamii na taasisi tofauti zikiwemo shule,” ilisema taarifa kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri Dkt Fred Matiang’i, Sicily Kariuki, Najib Balala, Amina Mohamed, Mwangi Kiunjuri, Simon Chelugui, na Eugene Wamalwa.