Habari

Hakuna pesa serikalini, Rotich aungama

March 8th, 2018 2 min read

DAVID MWERE na VALENTINE OBARA

Kwa ufupi:

  • Rotich asema uhaba wa fedha unaokumba serikali umesababishwa na kipindi kirefu cha uchaguzi pamoja na ukame
  • Hakueleza kwa nini serikali imeshindwa kukabiliana na ufisadi uliokithiri nchini na utumizi mbaya wa pesa za umma
  • Sh302 bilioni zilizopendekezwa kutengewa serikali za kaunti zitapunguzwa kwa kati ya Sh15 bilioni na Sh17 bilioni
  • Imebainika ni Sh134 bilioni pekee kati ya Sh302 bilioni zilizohitajika, zilikuwa zimesambazwa kwa kaunti 47 kufikia Jumatano

SERIKALI imekiri kuwa inakumbwa na upungufu wa fedha na hivyo haiwezi kutimiza mahitaji ya kaunti na ufadhili wa miradi ya maendeleo.

Hii inamaanisha kuwa baadhi ya miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara itasimama, vyombo vya habari kupunguziwa matangazo na mgao wa fedha serikali za kaunti kupungua ikilinganishwa na ilivyopangwa awali.

Akifichua hayo Jumatano, Waziri wa Fedha, Bw Henry Rotich alisema uhaba wa fedha unaokumba Serikali umesababishwa na kipindi kirefu cha uchaguzi mwaka uliopita pamoja na ukame, hali ambazo alisema zilifanya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) ishindwe kuafikia malengo yake.

“Tumeishiwa na pesa. Hali ya kisiasa nchini iliathiri vibaya biashara nchini. Hatuwezi kugawa kitu ambacho hatuna,” akasema Bw Rotich, alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti.

Haya yanajiri huku ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Pesa za Umma ikionyesha utumizi mbaya wa fedha za Serikali.  Kwa mfano ripoti ya majuzi zaidi ilifichua kuwa haijulikani jinsi Sh204 bilioni za mkopo wa Eurobond zilivyotumiwa.

Ripoti hiyo pia ilionyesha wabunge walioondoka walilipwa zaidi ya Sh569 milioni za usafiri bila kufuata mwongozo inavyohitajika.

Mbali na hayo, Wizara ya Elimu ilisemekana kutumia Sh231 milioni kununua tarakilishi 3,320 zilizonuiwa kupelekwa katika shule za upili, lakini ni tarakilishi 1,107 pekee ambazo zilifikishwa shuleni.

 

Miradi duni

Serikali za kaunti pia zilitajwa kutumia mamia ya mamilioni ya pesa kwa miradi duni na kwa matumizi ambayo hayaboreshi maisha ya wananchi kwa njia yoyote, kama vile usafiri na burudani.

Bw Rotich hakueleza kamati hiyo kwa nini serikali imeshindwa kukabiliana na ufisadi uliokithiri nchini na utumizi mbaya wa pesa za umma.

Waziri alisema Sh302 bilioni zilizopendekezwa kutengewa serikali za kaunti zitapunguzwa kwa kati ya Sh15 bilioni na Sh17 bilioni ili kuwezesha serikali kufadhili mahitaji mengine.

“Tunahitaji kushauriana nanyi maseneta pamoja na magavana ili tuweke wazi mambo ambayo hayawezekani kufanywa kwa kuzingatia changamoto zinazotukumba,” akasema.

Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior na Maseneta Maalum Rose Nyamunga na Fahriya Ali walipinga pendekezo la kupunguza mgao wa serikali za kaunti.

 

Serikali imepungukiwa

“Tuambie tu kuwa serikali imeishiwa! Kile unachotuambia kuhusu kupunguza mgao kwa serikali za kaunti ni jambo ambalo hatuwezi kukubali. Haiwezekani kufanya hivyo wakati uundaji wa bajeti nyingine tayari unaendelea,” akasema Bw Kilonzo.

Lakini Bw Rotich alishikilia msimamo wake kwamba serikali haiwezi kutumia pesa ambazo haina.

Mabadiliko hayo makubwa katika mgao wa fedha za umma yako kwenye bajeti ya pili ya ziada ambayo inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Taifa wakati wabunge watakaporejelea vikao vyao mapema wiki ijayo watakapokamilisha likizo fupi.

Miongoni mwa sehemu zitakazoathirika ni miradi ya maendeleo, ambayo waziri alisema inaweza kusubiri, na matumizi yasiyo muhimu kama vile usafiri, burudani na matangazo.

Waziri pia alikabiliwa na wakati mgumu katika kikao hicho kwani ilibainika ni Sh134 bilioni pekee kati ya Sh302 bilioni zilizohitajika, zilikuwa zimesambazwa kwa kaunti 47 kufikia Jumatano.

Bw Rotich alisema pesa zilichelewa kusambazwa kwa sababu ya marekebisho yaliyofanywa kwenye sheria ya ugavi wa fedha.