Hakuna Rais Mteule nchini kwa sasa, asema Raila

Hakuna Rais Mteule nchini kwa sasa, asema Raila

NA MWANDISHI WETU

RAILA Odinga wa Azimio La Umoja-One Kenya amepuuzilia mbali matokeo ya kura za urais yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati mnamo Agosti 15, 2022; akisema hakuna Rais Mteule nchini Kenya kwa sasa.

“Sisi Wakenya na wana-Azimio tunapenda amani. Tuko na mpango wa kuhakikisha tunamaliza changamoto ya ufukara na ukabila,” amesema Bw Odinga.

Amedai kwamba Bw Chebukati alichukua uamuzi ambao unakiuka msimamo wa makamishna wengi wa IEBC. Naibu Mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera, makamishna Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya jana Jumatatu walishikilia kwamba wanajitenga na matokeo yaliyotangazwa katika Ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi.

Vile vile makamishna hao wane leo Jumanne wamesema kwamba matokeo yaliyotangazwa yanaashiria asilimia 100.01 ambayo inapita asilimia 100. Aidha wamedai kwamba asilimia 0.01 inawakilisha karibu kura 142,000 ikizingatiwa wapigakura waliojitokeza ni zaidi ya 14 milioni. Ingawa hivyo, tathmini ya Taifa Leo inaonyesha kwamba 0.01 ni asilimia inayowakilisha kura karibu 1,420 pekee.

Katika matokeo yaliyotangazwa Jumatatu jioni na Bw Chebukati wa IEBC, Dkt William Ruto wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alipata kura 7,176,141 dhidi ya kura 6,942,930 za mpinzani wake wa karibu Bw Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance, hii ikiwa ni tofauti ya kura 233,211.Kulingana na Bw Chebukati, Dkt Ruto alipata asilimia 50.49 ya kura zote halali zilizopingwa huku Bw Odinga akipata asilimia 48.85.Dkt Ruto pia alipata zaidi ya asilimia 25 ya kura katika kaunti 39 huku Bw Odinga akipata asilimia sawa katika kaunti 34.

Profesa George Wajackoyah wa chama cha Roots Party aliibuka wa tatu kwa kupata kura 61,969 huku Bw David Mwaure wa chama cha Agano akiwa wa nne wa kura 31,987.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea na Tottenham watoshana nguvu katika gozi la EPL...

CHARLES WASONGA: Wizara ya elimu iongezee zaidi muda muhula...

T L