Hakuna ufadhili kwa mashirikisho ya michezo, wizara yasema imesota

Hakuna ufadhili kwa mashirikisho ya michezo, wizara yasema imesota

Na CECIL ODONGO

WIZARA ya Michezo, Utamaduni na Turathi za Kitaifa, kupitia Idara ya inayosimamia michezo, imeandikia mashirikisho ya michezo nchini kuwa haina fedha za kugharimia mashindano ya kimataifa kwa siku zilizosalia kwenye mwaka wa kifedha wa 2021/22.

Hii ni baada ya kutumia pesa zote zilizotengewa idara hiyo katika mwaka wa kifedha unaokamilika Juni 30. Badala yake, idara hiyo imeyataka mashirikisho hayo yasake msaada kutoka mashirika mengine ili kugharamia mashindano yao ya kimataifa.

“Idara ya serikali ya michezo ambayo imekuwa ikifadhili mashirikisho mbalimbali kwa mashindano ya kimataifa, haina uwezo wa kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu imetumia mgao wake wote katika mwaka huu wa kifedha,” ikasema barua iliyonakiliwa kwa mashirikisho yote.

“Ni kutokana na hilo ambapo ningependa kuarifu mashirikisho yote kuwa idara haina uwezo kufadhili mashirikisho hayo baada ya kumaliza mgao wake wa bajeti. Kwa wakati huu yanaombwa yasake ufadhili kutoka kwa mashirika mengine,” ikaongeza.

Katika mwaka wa kifedha wa 2021/22, idara ya kufadhili michezo ilitengewa Sh15 bilioni kutoka Sh1 bilioni mwaka uliotangulia. Katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2021/22, idara hiyo imetengewa Sh15.8 bilioni.

Kutokana na ukosefu huo wa fedha, Shirikisho la Raga tayari limeanza kukusanya pesa mitandaoni za kufaulisha safari zake mnamo Julai za kushiriki misururu ya mashindano ya Kombe la Dunia.

Malkia Strikers nao walifaa kuondoka nchini Jumapili kukita kambi Brazil japo bado hawajapokea Sh46 milioni wanazostahili kupokea kutoka kwa serikali kwa mujibu wa bajeti waliyowasilisha Aprili 1. Hata hivyo, timu hiyo sasa itaondoka leo baada ya kupokezwa ufadhili wa Sh10 milioni wiki jana kutoka kwa Mozzart Bet.

  • Tags

You can share this post!

Gor Mahia na Ingwe zavuna pakubwa kwa kupata mdhamini mpya

Bunduki 22, risasi 500 zapatikana katika nyumba mtaani...

T L