Habari

'Hakuna uhuru wa kuchapisha jumbe za mihemko na chuki'

October 7th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

VYOMBO vya habari vitabeba msalaba wavyo kwa chochote kinachochapishwa katika ana magazeti au kupeperushwa kupitia majukwaa yao mbalimbali kupasha taarifa ama kusambaza ujumbe unaoweza kuibua hisia za matusi au uchochezi.

Hii inamaanisha vyombo vya habari, watumiaji wa mitandao ya kijamii na wanasiasa wamedhibitiwa vilivyo ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuzima joto la kisiasa nchini.

Kwenye taarifa ya Baraza la Usalama Nchini, iliyosomwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua, onyo kali limetolewa Jumatano kwa vyombo vya habari na watumizi wa mitandao ya kijamii katika uenezaji wa jumbe zenye chuki, ukabila na zinazochochea ghasia au kuzua vurugu nchini.

Katika kikao na wanahabari Harambee House, jijini Nairobi, Bw Kinyua amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwajibika na kuwa makini katika habari au taarifa vinavyochapisha ama kupeperusha wakati huu ambapo kunashuhudiwa mihemko ya kisiasa.

“Vyombo vyote vya habari vitabeba msalaba wa taarifa zinazochapisha au kupeperusha. Visipeperushe wala kuchapisha jumbe zinazochochea chuki, ukabila au ghasia. Vijifunze kuripoti inavyopaswa, na kuhubiri amani,” Kinyua akaambia waandishi wa habari katika kikao nao, na ambacho hakikuwa na fursa ya kuuliza maswali pindi alipokamilisha kutoa taarifa hiyo.

Kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaosambaza jumbe na picha zinazochochea vurugu, wamepewa onyo na wakaagizwa wakome mara moja.

“Watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiwemo wadhibiti wa kurasa, watawajibikia jumbe, taarifa na picha wanazosambaza, ikiwa zinachochea ukabila, ghasia na ubaguzi wa kidini,” akaonya huku akihimiza vyombo vya habari na watumiaji wa majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii kwamba kabla ya kusambaza habari, ni muhimu kuthibitisha uhalisia wake. 

Akitoa onyo kwa wanasiasa, Bw Kinyua amesema asasi za usalama na zilizotwikwa jukumu kutathmini kinachochapishwa magazetini, kupeperushwa na pia kusambazwa mitandaoni, zitachukulia hatua kali wahusika.

Baraza la Usalama, linajumuisha Rais Uhuru Kenyatta, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Katibu katika Wizara hiyo, Dkt Karanja Kibicho, Inspekta Mkuu wa Polisi, IG Hillary Mutyambai, kati ya viongozi wengine wakuu wa idara za usalama nchini.

Taarifa ya Baraza hilo imejiri siku kadhaa baada ya ghasia zilizosababisha maafa ya watu wawili kushuhudiwa Kenol, Kaunti ya Murang’a, wakati Naibu Rais William Ruto alihudhuria hafla ya Kanisa la AIPCA katika eneo hilo.

Akilaani tukio hilo, Dkt Ruto hata hivyo alilaumu idara ya polisi kutumika na baadhi ya viongozi wakuu serikalini na pia wanasiasa.