Hakuna wa kunizuia kuwania ugavana Nairobi – Baba Yao

Hakuna wa kunizuia kuwania ugavana Nairobi – Baba Yao

Na STEVE OTIENO

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu, amepuuzilia mbali wanaosisitiza hafai kuwania ugavana Nairobi.

Akizungumza katika kikao cha wanahabari, Bw Waititu alisisitiza hajahukumiwa kwa uhalifu wowote na kwa hivyo ana haki ya kuwania kiti chochote cha kisiasa nchini.

“Ni kweli nilitimuliwa mamlakani Kiambu lakini madai yote dhidi yangu yalitolewa na maadui wangu walionitaja kuwa adui wa rais. Yote yaliyosemwa ni uongo. Hakuna anayeweza kunizuia kuwania kiti cha kisiasa,” akasema.

Bw Waititu aling’olewa mamlakani baada ya Seneti kukubaliana na madiwani wa Kiambu kwamba alipatikana na makosa ya kukiuka Katiba, kukiuka sheria za kitaifa na utovu mkubwa wa maadili.

Kinaya ni kwamba, anamezea mate kiti kilichobaki wazi baada ya aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko, ambaye alikuwa mwandani wake kwa muda mrefu, kutimuliwa kwa makosa yanayokaribiana na yake.

“Mimi nimelelewa Nairobi. Hapa ndipo nilisomea, nikafanya kazi nikiwa kijana. Nimewahi pia kuwa diwani hapa, naibu meya, mbunge wa Embakasi na hata nikawania ugavana 2013. Hapa ni nyumbani kwangu, ninafahamu kila kona,” akasema.

You can share this post!

WHO yatoa tahadhari ya corona kuleta kisonono sugu

BENSON MATHEKA: Polisi wakomeshe dhuluma kwa raia