Habari Mseto

'Hakuna zuio la watu kutoruhusiwa ama kuingia au kuondoka katika baadhi ya kaunti'

July 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali uvumi kwamba anapanga ‘kufunga nchi’ kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona, akisema hana mipango kama hiyo.

Akituhubutia taifa Jumatatu, Julai 27, 2020, baada ya kufanya mkutano na magavana, kiongozi wa taifa alifafanua kwamba kufunga nchi hakutakuwa na faida yoyote, lakini ni wajibu wa kila mwananchi kujilinda mwenyewe.

“Serikali haiwezi kumpa kila raia daktari; serikali haiwezi kuweka polisi wa kuchunga kila Mkenya. Nilivyosema siku 21 zilizopita, wajibu wa kupambana na ugonjwa huu ni wa kila mwananchi kama mtu binafsi. Jilinde na ulinde mama yako, baba yako, dada yako na mtoto wako,” akaeleza Rais Kenyatta akiwa katika Ikulu ya Nairobi.

Alisema kufungwa kwa nchi au kaunti kadhaa wakati huu hakutasaidia kupunguza kusambaa kwa virusi vya corona.

“Kufunga nchi hakutasaidia,” Rais Kenyatta akasema.

Tangu wiki jana kumekuwa na uvumi kwamba magavana nchini, wakiongozwa na mwenyekiti wao Wycliffe Oparanya, walitaka kwamba Rais afunge Kaunti ya Nairobi na zingine ambazo zimeandikisha ongezeko kubwa la idadi ya maambukizi.

Ilidaiwa kuwa watu kutoka katika kaunti hizi ndio wamekuwa wakisambaza virusi vya corona hadi kaunti zingine kwa kufanya safari za kila mara.