Hali ilivyo Kenya mwaka mmoja wa janga la Covid-19

Hali ilivyo Kenya mwaka mmoja wa janga la Covid-19

Na SAMMY WAWERU

MACHI 13, 2020, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza kuthibitishwa kwa mgonjwa wa kwanza wa Covid-19 nchini.

Ni ugonjwa ambao umegeuka kuwa janga la kimataifa, na ulioripotiwa kwa mara ya kwanza mjini Wuhan, China mwishoni mwa mwaka 2019.

Kisa cha kwanza kilifuatwa na cha pili, tatu, nne, tano… Mamia na kufikia Ijumaa, Machi 12, 2021 Kenya ilikuwa imeandikisha visa 111,935.

Jumla ya wagonjwa 1,901 wameangamizwa na virusi vya corona, huku waliothibitishwa kupona kabisa wakiwa 88, 209, kufikia jana.

Leo, Jumamosi, Machi 13, 2021, taifa linaadhimisha mwaka mmoja tangu Waziri Kagwe atangaze: “Tumethibitisha kisa cha kwanza cha mgonjwa wa virusi vya corona Kenya”.

Ni tangazo lililozua taharuki nchini, kutokana na habari tulizoskia na kutazama kwenye runinga mataifa yaliyoathirika.

Amerika, Uhispania, Uturuki, Italia na Ujerumani ni kati ya mataifa yaliyolemewa na janga la corona.

Takwimu zinaonyesha, kufikia sasa Amerika imeandikisha visa 29, 993, 423 vya maambuzi na maafa 545, 544.

Mwaka wa 2020, siku zilivyozidi kusonga ndivyo maambukizi yalizidi kuenea.

Kaunti ya Nairobi ilikuwa ya kwanza kuandikisha corona, ikafuatwa na Mombasa.

Ugonjwa huu sasa umegatuliwa, uko katika kila kaunti.

Uchumi uliyumbishwa, ambapo biashara ziliathirika, kuanzia sekta ya utalii, usafiri na uchukuzi, kilimo, hoteli, burudani, kati ya nyinginezo.

Sekta ya elimu na afya ziliathirika kwa kiasi kikubwa, shule zikifungwa kwa kipindi cha muda wa mwaka mmoja, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya Kenya.

Katika sekta ya afya, wahudumu kadha wa afya kuanzia madaktari, wauguzi na maafisa wa kliniki walifariki kutokana na makali ya corona.

Mbali na mashujaa hao, Covid-19 ilipokonya sekta ya sanaa na uigizaji staa, Charles Bukeko, maarufu kama Papa Shirandula, na viongozi na wanasiasa kadha.

Upungufu wa vifaakinga (PPE) pamoja na matakwa muhimu ulichochea madaktari, wauguzi na maafisa wa kliniki kushiriki mgomo wa kitaifa, kipindi ambacho taifa liliwahitaji kwa hali na mali.

Huku serikali ikijikakamua kufufua uchumi, ambao athari zake zimesababisha mamia ya maelfu nchini kupoteza ajira, Wakenya wanaendelea kuhimizwa kutii sheria na mikakati iliyowekwa na Wizara ya Afya kusaidia kuzuia msambao zaidi.

“Hata wakati tunaendelea kushughulikia kufufua uchumi, muhimu zaidi ni maisha ya Wakenya, lazima tuchukue tahadhari. Tuvalie barakoa, tunawe mikono na tuepuke kukongamana,” akahimiza Rais Uhuru Kenyatta kwenye hotuba yake kwa taifa Ijumaa.

Kafyu inaendelea kutekelezwa kote nchini kati ya saa nne za usiku na saa kumi asubuhi, kila siku.

Licha ya Kenya kuanza utoaji wa chanjo ya corona, visa vya maambukizi vimeonekana kuongezeka katika siku za hivi karibuni.

You can share this post!

Vipusa wa Manchester City wapewa Barcelona huku wa Chelsea...

Ndani ya miaka 50 ya huduma ya uchungaji kwa Askofu Peter...