Hali mbaya ya uchumi yatia hofu Wakenya wengi – Utafiti

Hali mbaya ya uchumi yatia hofu Wakenya wengi – Utafiti

Na WANDERI KAMAU

HALI mbaya ya uchumi, utawala mbaya na jinsi serikali inavyoshughulikia janga la virusi vya corona ni miongoni mwa masuala makuu yanayowafanya Wakenya kuhisi nchi inaelekea pabaya.

Hii ni kulingana na utafiti uliotolewa Jumapili na shirika la Infotrak, ulioonyesha kuwa kijumla, asilimia 65 ya Wakenya wanahisi nchi ina mwelekeo mbaya.

Asilimia 58 ya Wakenya walitaja kuhofishwa na hali mbaya ya uchumi, asilimia 15 utawala mbaya, huku asilimia 11 ikieleza kutoridhishwa na mikakati ya serikali kukabili maambukizi ya virusi hivyo.

Sababu nyingine zilizotajwa kuchangia hilo ni huduma duni za kijamii, hali mbaya ya miundomsingi na ongezeko la ukosefu wa usalama.

Utafiti huo unajiri wakati serikali ikiendelea kushinikizwa na Wakenya kutathmini upya athari za masharti ya kafyu, hasa katika kaunti za Nairobi, Machakos, Nakuru, Kajiado na Kiambu, ambazo zilifungwa na Rais Uhuru Kenyatta mwishoni mwa mwezi uliopita ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Hata hivyo, hatua hiyo imekosolewa na baadhi ya Wakenya na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za umma, yakisema inawaumiza badala ya kuwasaidia.

Ili kutatua hayo, baadhi ya masuala ambayo Wakenya wanataka yashughulikiwe kwa dharura ni gharama kubwa ya maisha (asilimia 20), ukosefu wa ajira (asilimia 18) na janga la virusi vya corona (asilimia nane).

Masuala mengine ni ufisadi, miundomsingi kama barabara na madaraja, huduma za afya, gharama za kuanzishia biashara, mikakati ya kupunguza umaskini kati ya mengine.

Utafiti ulionyesha asilimia 77 ya Wakenya wameathiriwa kwa namna moja au nyingine na janga la corona, huku asilimia 65 wakiunga mkono hatua ya serikali kuongeza muda wa kafyu katika maeneo mengine nchini.

Kulingana na ripoti hiyo, ni asilimia 14 pekee katika maeneo yote wanaohisi nchi ina mwelekeo mzuri.

Akitoa ripoti hiyo jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo, Bi Angela Ambitho, alisema hisia nyingi za Wakenya zimechangiwa na juhudi za serikali kukabili maambukizi ya corona, kiwango cha juu cha ufisadi serikalini na mazoea ya serikali kuchukua mikopo kutoka kwa mashirika ya kifedha ya kimataifa.

Alisema wengi walilalama kuwa gharama ya maisha iko juu sana baada ya serikali kurejesha kodi ambazo ilikuwa imetoa kama hatua ya kuwasaidia wananchi kukabili athari za virusi hivyo.

“Wakenya wengi wanataka hatua hiyo itathminiwe upya kama njia ya kuwasaidia kuhimili changamoto za kiuchumi zinazowakabili,” akasema.

You can share this post!

Pigo kwa Spurs fowadi Kane akiumia katika sare ya 2-2 dhidi...

Wataalamu wakiri kafyu ya mapema haina hata umuhimu