Makala

Hali ngumu ya maisha yalazimu mama kufanya kazi ya tuktuk akiwa na wanawe wachanga

January 20th, 2024 2 min read

NA FATUMA BUGU

KUPANDA kwa gharama ya maisha kulimshinikiza Bi Rehema Ali, kujitosa katika sekta ya usafiri na kuendesha tuktuk ili kukimu mahitaji ya famila yake.

Akiwa mama wa watoto wawili, aliikumbatia kazi hii baada ya kutengana na mumewe akidai kuachiwa majukumu si haba ya kuwalea wanawe. Alilazimika kuendesha tuktuk akiwahudumia wateja huku akiandama na wanawe wawili.

“Sina fedha za kutosha za kulipa kijakazi wa kukaa na wanangu inanibidi nitoke nao kila siku ninapoenda kazini,” akasema Bi Ali.

Kila uchao jua linapochomoza, Bi Ali huamka na kuandaa kiamsha kinywa na uji wa mwanawe kabla ya kuanza safari yake. Japo mara ya kwanza haikuwa rahisi, mwishowe alizoea.

“Mimi nimepitia maisha machungu mno tangu nilipojifungua mwanangu na baada ya siku saba nikaanza kazi. Singeweza kusalia nyumbani kwa kuwa sikuwa na wa kunisaidia. Watu hunishangaa njiani wengine ata hunitusi na kunikejeli ila sijali,” akasema Bi Ali.

Katikati ya jiji la Mombasa sasa ametambulika na kuapata umaarufu kwa kuendesha tuktuk akiwa na mwanawe mapajani huku mwengine akiwa ameketi kwenye kiti cha nyuma. Anakiri kuwa sio rahisi, kwani yeye hulazimika kuendesha tuk tuk kwa umakini.

“Ninapoiendesha tuktuk lazima niwe mwangalifu nisije nikamuumiza mtoto hasa ninaporudi nyuma na kukata kona,”anaongeza.
Ni hali iliyomfanya kukamatwa mara kadhaa kwa kosa la kuendesha tuktuk akiwa na watoto wake.

“Nilipelekwa hadi kortini ila nikajitetea na kuachiliwa kwa sababu sijui watoto wangu wataishi vipi bila kazi hii kwa kuwa ndio kila kitu,”anaeleza Bi Ali.

Kwa wengi hatua hii ni ya kijasiri na anahoji kuwa wengi wanapomwona hupenda kuipanda tuktuk yake, ila kwa baadhi taswira ni tofauti.

”Kuna wengine wakiniona tu hata hawaniangalii mara mbili , kuna yule nitambeba anisaidie kumbeba mtoto na kuna wale ambao hata kuguzwa na mwanangu hawataki lakini navumilia ndo wanaotupa pesa,” akasema Bi Ali.

Mara nyingi anaeleza kuwa anapopata wateja kama hao, hulazimika kumtuliza mwanawe asiwasumbue abiria ili wapate riziki.

Kulingana naye, kazi hiyo haikosi changamoto akidai kuwa kejeli na kurukwa katika mpangilio wa tuktuk na wanaume wanaofanya kazi naye humuumiza mno.

“Wakati mwengine huniona mnyonge na wananipita kwenye foleni ya mpangilio wa kujaza abiria wengine wananitukana, ” akasema Bi Ali.

Mwendeshaji tuktuk Bw David Wanjala, mwendeshaji tuktuk ni miongoni mwa wanaume ambao wamewakubali na kuwakumbatia wanawake wanaojichumia riziki ila anahofu juu ya hali ya Bi Ali.

“Ni vyema anavyojikakamua ila sioni ni sawa kupeleka tuktuk ama kifaa chochote cha usafiri ukiwa umeshikilia mtoto ni hatari mno, barabarani kuna mengi,”anasema Bw Wanjala.

Ndoto yake ni kumiliki tuktuk yake binafsi itakayo mwezesha kuweka akiba ya kutosha.

“Kwa sasa lazima nitafute Sh800 hadi 1000 za aliyeniajiri. Wakati mwengine mimi hukosa, nikipata yangu najua ntakachokuwa napata naweka nile na wanangu,” alisisitiza Bi Ali.

Aidha, licha ya dhuluma anazopitia, anaifurahia kazi yake akiwapa wosia wanawake wenzake wajizatiti kujitafutia riziki bila kutegemea mtu yeyote.