Michezo

Hali tete kambini mwa Ubelgiji makipa wote tegemeo wakiondoka kambini kabla ya kuvaana na Uingereza na Iceland

October 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MAANDALIZI ya Ubelgji kwa mechi ya Uefa Nations League itakayowakutanisha na Uingereza uwanjani Wembley mnamo Oktoba 11, 2020 yamevurugika.

Hii ni baada ya mlinda-lango wa Real Madrid, Thibaut Courtois kuwa kipa wa tatu kujiondoa kambini mwa Ubelgiji ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Roberto Martinez.

Kabla ya mechi ya kirafiki iliyokutanisha Ubelgiji na Ivory Coast mnamo Oktoba 8, 2020, ilikuwa imethibitishwa kwamba Courtois, 28, angalikuwa sehemu ya kikosi ambacho kingetegemewa na Martinez dhidi ya Uingereza.

Hata hivyo, mlinda-lango huyo wa zamani wa Chelsea aliondoka kambini mwa Ubelgiji mnamo Oktoba 9, baada ya kupata jeraha la paja.

Hadi kujiondoa kwa Courtois, kocha Martinez alikuwa pia ameaga kipa Hendrik Van Crombrugge wa Anderlecht (Ubelgiji) na Koen Casteels ambaye kwa sasa anawadakia VfL Wolfsburg ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Crombrugge na Casteels walirhusiwa kuondoka kambini mwa Ubelgiji usiku wa Oktoba 8, ili kuwa na wake zao waliokuwa wakitazamiwa kujifungua.

Hali tete kwenye idara ya ulinzi wa lango la Ubelgiji sasa ilimsukuma kocha Martinez kumwita kambini kipa wa zamani wa Liverpool, Simon Mignolet, 32, kwa minajili ya mechi dhidi ya Uingereza.

Mbali na Mignolet ambaye pia amewahi kuchezea Sunderland, makipa wengine ambao Martinez anatazamia kuripoti kambini kufikia Oktoba 9, 2020 ni chipukizi Davy Roef na Jens Teunckens.

Courtois alikuwa sehemu ya wanasoka wa haiba kubwa zaidi wakiwemo Toby Alderweireld, Kevin De Bruyne, Romelu Lukaku na Axel Witsel ambao Martinez alitazamia kuwachezesha dhidi ya Uingereza.

Baada ya kuvaana na Uingereza, Ubelgiji watashuka dimbani kuchuana na Iceland kwenye gozi jingine la Nations League mnamo Oktoba 14.

Kati ya wanasoka 33 ambao kocha Martinez aliwaita kambini kwa minajili ya mechi hizo mbili ni tineja wa AC Milan nchini Italia, Alexis Saelemaekers na kiungo chipukizi wa Brighton ya Uingereza, Leandro Trossard.