Michezo

HALI TETE: Roho mkononi Spurs wakialika Bayern Uefa

October 1st, 2019 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

TOTTENHAM Hotspur watakuwa leo Jumanne wenyeji wa Bayern Munich katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambao wanalazimika kushinda ili kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya 16-bora bila presha ya dakika ya mwisho.

Katika michuano mingine, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Manchester City watawaalika GNK Dinamo Zagreb ya Croatia huku Real Madrid wakivaana na Club Brugge ya Ubelgiji uwanjani Santiago Bernabeu, Uhispania.

Lokomotiv Moscow kutoka Urusi watamenyana na Atletico Madrid mbele ya mashabiki wao wa nyumbani, Leverkusen wawaendee Juventus jijini Turin, Italia huku PSG wakiwa wageni wa Galatasaray nchini Uturuki.

Kinyume na Bayern waliowapepeta Red Star Belgrade 3-0 katika mchuano wao wa kwanza nchini Ujerumani, Tottenham walilazimishiwa sare ya 2-2 na Olympiacos nchini Ugiriki.

Bayern ambao wamejivunia ukiritimba wa soka ya Ujerumani kwa kipindi kirefu watajibwaga ugani wakijivunia kupigwa jeki na marejeo ya wavamizi Lucas Hernandez na Ivan Perisic ambao kocha Nico Kovac amefichua kwamba atawapanga katika kikosi cha kwanza.

Hernandez aliondolewa uwanjani katika kipindi cha kwanza dhidi ya Paderborn mnamo Jumamosi baada ya kuanza kuhisi maumivu kwenye goti lake la kulia.

Japo alitarajiwa kusalia mkekani kwa kipindi kirefu zaidi, madaktari walimruhusu kushiriki vipindi viwili vya mazoezi mnamo Jumapili.

Kwa upande wake, Perisic alikosa mechi dhidi ya Paderborn kutokana na mafua. Hata hivyo, kwa sasa ameruhusiwa kuunga kikosi kitakachoelekea Uingereza kwa kibarua kizito dhidi ya Tottenham.

Perisic na Hernandez waliojiunga na Bayern msimu baada ya kuagana na Inter Milan, walikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Bayern kilichochuana na Red Star Belgrade. Mabao ya Bayern katika mchuano huo yalifumwa wavuni na Kingsley Coman, Robert Lewandowski na Thomas Muller.

Bayern na Spurs ni vikosi viwili vinavyopigiwa upatu wa kutawala kilele cha Kundi B na kusonga mbele kwa hatua ya 16-bora. Presha ya kudumisha uhai wa matumaini hayo ni jambo ambalo linatarajiwa kumkosesha kocha Mauricio Pochettino usingizi.

Chini ya Pochettino, Spurs walitinga fainali ya UEFA msimu jana ila wakazidiwa maarifa na Liverpool ambao walizamishwa 2-0 na Napoli katika mchuano wao wa kwanza.

Hivyo, ushindi kwa Bayern katika mchuano wa leo utawasaza Spurs pabaya zaidi kundini na katika hatari ya kuondolewa mapema sawa na walivyoshuhudia katika kivumbi cha Carabao Cup wiki iliyopita baada ya kudenguliwa na limbukeni Colchester.

Matokeo duni ya Spurs tangu mwanzoni mwa msimu huu kwa sasa yanamweka Pochettino katika hatari ya kutimuliwa huku waajiri wake wakifichua mipango ya kumpokeza mikoba kocha Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza.

Dalili zote zinaashiria kwamba Pochettino anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Manchester United, yuko tayari kuagana na Tottenham baada ya kuanza kuwa na mazoea ya kuwalaumu wachezaji wake kila mara kikosi kinaposajili matokeo duni.

Ni mara ya pili kwa Spurs kuziwania huduma za Southgate, 49, hasa ikizingatiwa kwamba waliwahi kuyataka maarifa ya mkufunzi huyo kwa mara nyingine mwishoni mwa msimu uliopita.

Hatua hiyo ilichochewa na suitafahamu kuhusu mustakabali wa Pochettino aliyekuwa akiandamwa sana na Real Madrid huku naye akisitasita kusalia Spurs kwa mwaka wa tano.

Ubovu wa mbinu

Baadhi ya wachezaji waliotaka kuondoka Spurs mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuchoshwa na ‘ubovu wa mbinu’ za ukufunzi za Pochettino ni Christian Eriksen, Danny Rose na Toby Alderweireld.

Chini ya Southgate, makali ya nyota Harry Kane, Dele Alli, Harry Winks, Danny Rose na Eric Dier yameimarika sana kiasi kwamba kwa sasa ndio tegemeo kubwa kambini mwa Tottenham.

Huku Bayern wakiselelea kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 14 kutokana na mechi sita hadi kufikia sasa, Tottenham wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 11 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na viongozi Liverpool ambao hawajapoteza mchuano wowote kati ya saba ya ufunguzi wa kampeni za msimu huu.

Zaidi ya kutegemea maarifa ya Perisic, Bayern wanatazamiwa pia kuchuma nafuu kutokana na ukubwa wa ushawishi wa mshambuliaji Robert Lewandowski anayetarajiwa kushirikiana vilivyo na sajili mpya Philippe Coutinho aliyetokea Barcelona kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu.

Bayern na Tottenham wamewahi kukutana mara nne katika mapambano ya awali ya Uefa.

Miamba hao wa soka ya Ujerumani walipokeza Spurs kichapo cha jumla ya mabao 5-2 katika kivumbi cha Uefa Cup Winners Cup mnamo 1982. Walipokutana tena katika raundi ya tatu ya Uefa Cup mnamo 1983-84, Spurs waliwalaza Bayern kwa jumla ya magoli 2-1.

Walipepetana tena katika kivumbi cha Audi Cup kilichoshuhudia Tottenham wakisajili ushindi wa 5-4 kupitia mikwaju ya penalti.