Habari Mseto

Hali ya usalama yazorota Mombasa

August 13th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WAKAZI Mombasa wana taharuki kufuatia kuongezeka kwa visa vya utovu wa usalama mjini humo.

Wakazi hao walisema kumezuka genge la majambazi wanaotumia bunduki kuvamia wafanyabiashara.

Walitaja maeneo ya Changamwe, Likoni, Kisauni na Mombasa Mjini kuwa ndiyo yanaongoza kwa visa vya utovu wa usalama.

Kulingana nao, majambazi hao ambao wamekuwa wakiwavamia wahudumu wa Mpesa, kuvunja majumba na hata kuvamia magari ya wamiliki binafsi mchana.

“Wanatumia pikipiki kutoroka baada ya kuvamia na kunyang’anya watu mali zao,” akasema mfanyakazi katika eneo hilo Bw Alphone Masese.

Walisema hayo baada ya kusambaa kwa video ya CCTV ya marehemu Winnie Ambesa aliyekuwa akihudumu katika duka la Mpesa eneo la Express mjini Mombasa. Aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi wawili ambao walitoroka na mfuko wake.

Mkazi mwingine Bw Juma Omar, alisema majambazi hao pia huvamia watu katika magari yao kukiwa msongamano.

“Kuna baadhi yao husubiri eneo la Mwembe Tayari nyakati za jioni na asubuhi kukiwa na msongamano. Hujiingiza ndani ya magari kisha kuwapora wamiliki,” akasema.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya wafanyabiashara kuanza kufunga biashara zao mapema kwa kuhofia uhai wao.

Mkuu wa polisi mjini humo Bw Eliud Monari alisema maafisa wa polisi wanawasaka majambazi wawili waliomuua Bi Ambesa.

“Tunafuatilia wawili waliomuua mhudumu wa Mpesa Bi Ambesa. Tutahakikisha tunawanasa wawili hao pamoja na wenzao wote wanaoshirikiana nao katika uhalifu. Pia tunaomba aliye na habari kuwahusu atufahamishe,” akasema.