Habari Mseto

Halmashauri yazindua mkakati wa kuboresha huduma za maji

August 21st, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

HALMASHAURI ya Usimamizi wa Mto Athi (AWWDA) imezindua Mkakati wa Utendakazi wa Miaka Mitano, unaolenga kuimarisha huduma na idadi ya watu wanaopata maji chini ya usimamizi wake.

Mkakati huo, ukaotekelezwa kati ya mwaka 2019 na 2024 vile vile unalenga kuongeza idadi ya watu wanaopata maji safi katika eneo linalosimamia.

Akihutubu Jumanne kwenye hafla yauzinduzi wa mkakati huo jijini Nairobi, Waziri wa Maji Simon Chelugui alisema kuwa juhudi kama hizo ndizo zitawahakikishia Wakenya huduma bora za maji.

“Mikakati kama hii ni muhimu kwani inaonyesha kwamba Kenya bado inapiga hatua muhimu kwenye juhudi za kuhakikisha kuwa kila Mkenya amefikiwa na maji safi bila kujali mahali alipo,” akasema Bw Chelugui.

Waziri wa Maji Simon Chelugui akihutubu kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Utendakazi wa Halmashauri ya Maji ya Mto Athi, Nairobi. Picha/ Wanderi Kamau

Baadhi ya malengo ya halmashauri hiyo inalenga kutimiza kufikia mwaka 2024 ni kuongeza idadi ya watu wanaofikiwa na maji katika eneo inalosimamia kutoka asilimia 72 hadi 80, kuongeza idadi ya watu wanaopata maji safi kutoka asilimia 47 hadi 70, kuimarisha shughuli za kuongeza mapato kufikia Sh234.8 bilioni, kuongeza utafiti na ukumbatiaji wa teknolojia na kuimarisha mfumo wake wa uongozi.

Halmashauri hiyo inakita malengo yake kwenye Sheria ya Maji ya 2016, ambayo inatoa taratibu zinazopaswa kuzingatiwa na asasi za maji kuimarisha huduma zinazotoa kwa wananchi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa hamlashauri hiyo Mhandisi Michael Thuita alisema kuwa mkakati huo unalingana na Ajenda Nne Kuu za Maendeleo za Serikali ya Jubilee.

“Rais Uhuru Kenyatta ametilia mkazo sana suala la maji, kwani ni miongoni mwa matatizo makuu yanayowakumba Wakenya. Tunatarajia kuwa kwa mkakati huu, halmashauri na asasi zingine zinazosimamia masuala ya maji zitaweka juhudi kuboresha huduma zao,” akasema Bw Thuita.

Halmashauri hiyo ni miongoni mwa zingine nane nchini ambazo zimebuniwa chini ya Wizara ya Maji.

Inasimamia masuala ya maji katika kaunti za Nairobi, Kiambu na Muranga, ambazo zina zaidi ya watu milioni nane.

Halmashauri hiyo ilibuniwa mnamo 2003. Wengine waliohutubu ni Naibu Waziri wa Maji Bi Winnie Guchu.

Kenya inaorodheshwa kuwa miongoni mwa nchi zinazokumbwa na uhaba wa maji duniani na serikali imekuwa ikiweka juhudi kuongeza idadi ya Wakenya wanaofikiwa na huduma za maji.