Kimataifa

Hamasisho wanaume wavae minisketi

June 25th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

MAONYESHO ya urembo Paris yaliyokamilika Jumapili yalibainisha juhudi za kuhamasisha wanaume kuvaa mavazi yoyote wapendayo, hata kama ni minisketi. 

Wasanii wa mitindo ya urembo na kimavazi walitaka kuonyesha kuwa katika enzi hizi, wanaume hawafai kufungwa pingu kuhusu kile wanachostahili kuvaa.

Mavazi ya wanaume yaliyoibuka kwenye maonyesho hayo ni mavazi yenye michoro ya maua, suti za rangi ya waridi, sketi na marinda.

Ingawa kuna mataifa ambapo ilikuwa kawaida kwa wanaume kuvaa sketi katika miaka ya jadi, haijakuwa kawaida kwa wanamitindo kuhamasisha mavazi hayo yakumbatiwe kimataifa katika jamii.

“Suala la jinsia halijalishi kamwe enzi hizi, tuko katika mwaka wa 2018,” akasema msanii mashuhurii wa mitindo ya kimavazi Kim Jones.

Msanii mwingine, Vuitton Jones, alisema ni wakati wa ulimwengu kuzika “ubaguzi” wa kimitindo katika kaburi la sahau na kuacha watu wavae jinsi watakavyo.

-Imekusanywa na Valentine Obara