Michezo

Hamilton ampiku Schumacher kwenye mbio za magari ya Langalanga

October 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LEWIS Hamilton aliweka historia kwa kuibuka mshindi bora wa muda wote wa mashindano ya mbio za magari ya Langalanga (Formula One).

Hii ni baada ya kusajili ushindi wa 92 katika mashindano ya Grand Prix, duru ya Ureno mnamo Oktoba 25 na kumpiku nguli Michael Schumacher.

Kwa kuzitawala mbio hizo, Hamilton aliivunja rekodi ya miaka 14 ya Schumacher alisajili ushindi mara 91 tangu atamalaki mbio za kwanza za F1 za Algarve Circuit.

“Hongera Lewis kwa kuingia katika mabuku ya kihistoria!” akasema kinara wa magari ya Mercedes, Toto Wolff na kumalizia kwa “92 Lewis, 92”.

Hamilton alijitahidi maradufu baada ya kuonekana kulemewa awali alipotupwa hadi nafasi ya tatu gari lake lilipopata tatizo la gurudumu kutokana na mvua.

Ushindi alioupata nchini Ureno mnamo Oktoba 24 ulikuwa wake wa nane katika jumla ya mashindano 12 ambayo ameyanogesha mwaka huu.

Hamilton ambaye ni bingwa mara sita wa dunia, alikamilisha mbio hizo kwa sekunde 25.5 mbele ya mwenzake wa Team Mercedes, Valtteri Bottas. Max Verstappen wa Red Max aliridhika na nafasi ya tatu.

Hamilton kwa sasa anajivunia rekodi ya kuibuka wa kwanza mara 97, kutwaa medali katika mashindano 161 kwa idadi kubwa ziadi ya alama (45 mfululizo).

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 aliendeleza rekodi yake ya ushindi dhidi ya Bottas kwa alama 77.

Kufikia sasa, dalili zote zinaashiria kwamba Hamilton ataivunja rekodi ya Schumacher anayejivunia mataji saba ya dunia. Hii ni kwa sababu zimesalia mbio tano zaidi kabla ya kampeni za msimu huu kukamilika rasmi.

Charles Leclerc aliyekuwa akiendesha Ferrari aliambulia nafasi ya nne mbele ya Pierre Gasly (Alpha Tauri). Carlos Sainz (McLaren) aliibuka wa sita baada ya kumpiku Sergio Perez (Verstappen) aliyemaliza mbele ya Esteban Ocon na Daniel Ricciardo (wote Renault). Bingwa mara nne wa dunia, Sebastian Vettel (Ferrari) aliambulia nafasi ya 10.