Makala

Hamna tatizo mtoto wa kiume kutumia jina la mama, mzee wa Agikuyu asema

April 30th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWENYEKITI wa kundi la Kiama Kia Ma katika jamii ya Agikuyu tawi la Nairobi, Bw John Mugwe Wanjuhi, ameweka bayana kuwa hakuna tatizo, wanaume wa jamii hiyo kutumia jina la mzazi wa kike.

Bw Mugwe alisema huo ni utambulisho tosha kuwa mwanaume huyo ana familia inayomthamini.

Wiki jana, mhubiri wa injili Bw Robert Burale alikosoa vikali jinsia ya kiume kutumia jina la tatu ambalo huwa la kike.

Bw Mugwe alifafanua kuwa sababu ya kwanza mwanaume kutumia jina la mamaye ni kutokana na mzazi wa kiume kukosa kujitokeza na kumtafuta mwanawe. Alikemea baadhi ya wanaume ambao hukwepa mimba za wapenzi wao na kuachia wanawake jukumu la kulea pekee yao.

“Iwapo baba hajulikani basi mtoto hana namna nyingine ila kutumia jina la mama pekee. Kuna kipindi ambacho kama baba anayekisiwa hupewa ili ajitokeze na kusema huyu ni mtoto wangu,” alieleza Bw Mugwe.

“Akikosa kujitokeza, mtoto anabaki kuwa ni wa familia ya akina mama. Ndio maana wengi wa wanaume kutoka jamii yetu watapewa shamba la kufanya maendeleo ujombani,” alisema Bw Mugwe.

Hata hivyo, kuna jinsi jamii hiyo ya Agikuyu humpa mtoto jina anapozaliwa. Bw Mugwe alisema mtoto wa kwanza na wapili kwenye familia hupewa majina ya upande wa akina baba.

Mzee wa Agikuyu John Mugwe Wanjuhi baada ya mazungumzo na Taifa Leo jijini Nairobi| PICHA| FRIDAH OKACHI

“Kifungua mimba na anayemfuata hupewa jina la babu au nyanya. Wanaofuata hupewa jina kutoka kwa familia ya mama.”

Je, iwapo, mwanamke alipata mtoto kabla ya ndoa, jamii ya Agikuyu hufanya vipi?

“Kama mtoto alizaliwa kabla ya mama kuolewa na anahitaji kurudi kwa baba mtoto, jambo la kwanza ni lazima atakaswe. Ikiwa pia, wakati baba alipeana mimba na mama akasusia kwenda kuishi huko, basi anaadhibiwa na wazee wa jamii kwa kutoa mbuzi,” alifafanua Bw Mugwe.

Hata hivyo, baadhi ya vijana kutoka kwenye jamii hiyo, wametoa sababu zao za kujumuisha jina la mama kwenye stakabadhi muhimu. Bw John Machari Wanjiru, 29, aliyezungumza kwa uchungu na Taifa Leo Dijitali, alimkosoa vikali, mhubiri huyo, akisema kuwa katu hawezi kutumia jina la baba ambaye hajawahi kujukumika kwenye maisha yake.

“Mbona nitumie jina la mtu ambaye hajawahi kujitokeza kwenye maisha yetu?” aliuliza Bw Macharia.

Mkazi huyo kutoka Nairobi alisisitiza kuwa japo ni miaka 29 sasa, hawezi kubadilisha jina iwapo atamfahamu babake kwa sasa.

“Nikiwa na umri mdogo, sikuwahi kumuona baba mzazi. Nilisikia uvumi hapa kitambo kuwa babangu alikuwa mwalimu. Nasema tena siwezi kutumia jina la ambaye hakujukumika kwenye malezi yangu,” aliongeza.

Bi Christine Wanjiru, alihadithia jinsi alimfahamisha kuhusu na kutaka wakutane. Ni ombi ambalo mzazi mwenza alisusia.

“Kinachoumiza sana umejaribu kadri ya uwezo wako wawili hawa wapatane ila kunakuwepo na pingamizi.”

“Pia, hakuna mahakama ambayo itamlazimisha mwanao atumie jina lako ambalo hapo awali hukutaka,” alisikitika mzazi huyo.

Mzazi huyo aliambia Taifa Leo, wanawe wamemfahama kuwa mzazi wa kipekee kwa kuwashughulikia. Na wanapohitaji kuchukua stakabadhi ambazo wafaa kutumia jina la baba, walitumia jina lake.