Habari

Hamning'oi kitini, Ruto ajibu wabaya wake

March 14th, 2020 2 min read

TOM MATOKE na WYCLIFF KIPSANG

NAIBU Rais William Ruto, Ijumaa alipuuzilia mbali mpango wa mahasimu wake kisiasa kutaka kumbandua mamlakani, akisema kuwa hawatafanikiwa.

Alisema hayo wakati wafuasi wake waliokuwa wakiandamana mjini Eldoret bila idhini ya polisi kueleza kughadhabishwa kwao na mpango huo wa kumbandua, walikabiliwa vikali na polisi na kutawanywa kwa vitoa machozi.

Dkt Ruto alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Nandi ambapo alizindua miradi kadhaa na kuwaambia wabunge wanaopanga kumbandua kuwa wanafanya kazi ya bure.

Alisema kuwa juhudi hizo zitafanikiwa tu kuitatiza serikali ya Jubilee isitimize ahadi ilizotoa kwa Wakenya katika uchaguzi uliopita.

“Nawashauri wanaopanga kunibandua huko Nairobi kuwa mipango yenu ya kichinichini haitawafikisha popote. Mnafaa kurudi kuwahudumia waliowachagua kwani huko kunibandua mnakonipangia kunaweza kuwarudia mkabanduliwa na wananchi,” akasema alipokuwa eneo la Mosop ambapo alikuwa akipeana hati za umiliki wa ardhi.

Vilevile, Dkt Ruto aliwapuuzilia viongozi ambao wamekuwa wakimkosoa kuwa anamkosea Rais Uhuru Kenyatta heshima, akisema wana malengo yao ya kibinafsi.

“Viongozi waache kuwa wakora na waongo. Tuhakikishe tunatenda tuliyowaahidi wananchi. Bado mimi na Rais tunafanyia watu wetu kazi,” Dkt Ruto akasema.

Viongozi wanaomkosoa wamekuwa wakidai kuwa Dkt Ruto ameleweshwa na azma ya Urais katika uchaguzi wa 2022, badala ya kuwahudumia Wakenya.

“Mimi kama msaidizi wa Rais, ninafahamu kile nilichaguliwa kufanya. Watu wengine wanadhani nikienda mahali ninaenda kupiga siasa. Sijakuja hapa Nandi kupiga kampeni, huo wakati utafika,” akasema.

“Nasikia wengine wakisema ninapiga kampeni. Bado sijaanza. Bado namsaidia Rais kutekeleza ajenda alizowaahidi Wakenya, na ninafanya hivyo jinsi inatarajiwa,” akaongeza.

Lakini viongozi walioandamana naye walionekana kupiga vita Mpango wa Maridhiano (BBI) ulioanzishwa na Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“BBI na reggae ni ngeni kwetu. Hatuko tayari kwa reggae, bado tunashughulika na agenda nne kuu, kutekeleza miradi ya maendeleo na kuhudumia watu wetu,” akasema Gavana wa Nandi Stephen Sang.

Dkt Ruto yuko katika ziara siku chache ngome yake ya kaskazini mwa bonde la ufa, na leo anatarajiwa kaunti za Trans Nzoia na Pokot Magharibi.

Mjini Eldoret nako, polisi walilazimika kutumia gesi za kutoa machozi kutawanya kikundi cha wafuasi wa Dkt Ruto ambao walikuwa wakiandamana, kutaka aheshimiwe na wanaoongoza BBI.

Waandamanaji hao ambao walikuwa wakiimba nyimbo za kukashifu BBI walikashifu mchakato mzima wa kuendesha mikutano yake kuwa imebadilishwa kuwa ya kisiasa.