Hamwezi kuzima hasla, Ruto aambia wapinzani

Hamwezi kuzima hasla, Ruto aambia wapinzani

BENSON MATHEKA NA PIUS MAUNDU

NAIBU Rais William Ruto amewasuta viongozi wa vyama vya upinzani akisema wanajuta kwa kudharau kampeni yake ya kuinua uchumi wa Wakenya wa tabaka la chini, hasla, akisema wameshindwa kuizima.

Dkt Ruto alisema wapinzani wake wamegundua kwamba hawawezi kuzima kampeni hiyo, na sasa wameanza kuzungumzia masuala ya uchumi badala ya mabadiliko ya Katiba.

“Tulipoanza kuzungumza kuhusu raia, walipuuza nilipowaambia kuwa serikali ya 2022 itaundwa na mahasla. Lazima tuanze kujadili masuala ya watu wa matabaka ya chini. Hii ndiyo sababu tulisema kuwa tutabadilisha mjadala kama Wakenya,” Dkt Ruto alisema alipokutana na wachuuzi pamoja na wafanyabiashara wadogo mjini Machakos.

Naibu Rais alihoji kuwa alipoanza kampeni yake wapinzani wake walisema ilikuwa ya kuchochea masikini dhidi ya matajiri; na sasa kwa vile imefaulu, wameshtuka.

Aliongeza kuwa alipokuwa akikutana na Wakenya wa matabaka ya chini kujadili jinsi ya kuimarisha uchumi wao, wapinzani wake walikuwa wakijadili jinsi ya kubadilisha Katiba ili kubuni nyadhifa zaidi za uongozi.

“Sasa wanakutana katika kumbi wakijadili watakavyounda miungano ya kisiasa na kugawa nyadhifa sisi tukisaidia mahasla kuimarisha uchumi ili kuwezesha kila mtu,” akasema.

Dkt Ruto alikuwa akigusia viongozi wa vyama vya Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi wa ANC, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu, ambao wamekuwa wakikutana kusuka muungano wao wa One Kenya Alliance (OKA).

Chama cha ODM, chake waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, nacho kimekuwa kikifanya mazungumzo na muungano tawala wa Jubilee wake Rais Uhuru Kenyatta, kwa lengo ya kuungana kabla ya uchaguzi mkuu 2022.

Hata hivyo, mazungumzo kati ya ODM na Jubilee yamesitishwa kwa wakati huu.Dkt Ruto ambaye amekuwa akipinga mchakato wa kubadilisha Katiba, kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) uliotokana na handisheki ya Rais Kenyatta na Bw Oding, alisisitiza Katiba haitabadilishwa.

“Reggae ilisimama. Ninawahakikishia kwamba hatutabadilisha Katiba, tutabadilisha uchumi,” akaeleza.

Naibu Rais alikuwa ameandamana na mbunge wa Machakos Mjini Bw Victor Munyaka, Nimrod Mbai wa Kitui Mashariki na Vincent Musyoka wa Mwala.

Alisema handisheki na BBI zilivuruga ajenda ya maendeleo ya serikali ya Jubilee.“Mpango wetu wa mwaka 2018 ulihusu ujenzi wa makazi ya bei nafuu, ukuzaji kilimobiashara, afya kwa wote, ustawi wa viwanda na elimu kwa watoto wetu.

“Lakini baadhi ya watu walijiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma na kutuambia kuwa mipango hiyo haikuwa ya haraka. Walituambia dharura ilikuwa ni mradi wa kubadilisha Katiba ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka minne sasa. Mungu amekuwa upande wetu na reggae imesimama,” akajipiga kifua Dkt Ruto.

Kiongozi huyo anayeegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA), amekuwa akisusia hafla za Rais Kenyatta tangu atengwe serikalini kwa kupinga handisheki.Mjini Machakosa alisema baadhi ya viongozi wanagawa Wakenya kwa makabila.

“Nataka kuwaambia kwamba Wakenya wanajua shida yao si makabila, Katiba au nyadhifa. Bali uchumi unaodorora, na ili kukabiliana na hali hii lazima tuanzie mashinani,” akasema.

.Aliwasuta viongozi wa upinzani Raila Odinga na Bw Musyoka akiwataka waombe Wakenya msamaha “kwa kujiunga na serikali kinyume cha sheria.”

Wawili hao wamekuwa wakiunga BBI na wamepatiwa majukumu ya kimataifa.

You can share this post!

Desturi ya aina yake kisiwani Lamu inayozipatia mashua...

Pigo kwa afisa korti kuunga uamuzi wa gavana kumfuta