Shangazi Akujibu

Hana haraka ya kunioa rasmi japo aliahidi nikishajifungua

April 30th, 2024 1 min read

Shangazi;

Hujambo. Nilianza kuishi na mpenzi wangu miaka miwili iliyopita baada ya kunipa mimba. Alikuwa ameniahidi tutaenda kwa wazazi wangu lakini naona hana haraka. Nishauri.

Mlikiuka maadili ya ndoa kwa kuoana bila kuhusisha wazazi. Ni hatari kuishi na mwanamume huyo ilhali wazazi wako hawamjui. Mpe hilo kuwa sharti la kuendelea kuishi naye la sivyo muachane.

Ameanza kulala nje bila sababu za maana

Mume wangu ameanza tabia ambayo inatishia ndoa yetu ya miaka miwili. Kuna wakati analala nje nikimuuliza anazua ugomvi. Nifanye nini?

Hali kwamba mume wako anazua fujo ukilalamika ni ishara kwamba kuna mambo mabaya anayoshiriki akilala nje. Kama hataki kujirekebisha itakuwa hatari kuendelea kuishi naye.

Nimezamia ponografia sababu sina mshikaji

Nina miaka 30 na sijawahi kuwa na mpenzi. Nimekuwa nikituliza hisia za kimapenzi kwa kutazama video za ngono mtandaoni. Nahofia tabia hiyo itanifanya nisione haja ya kuwa na mpenzi. Nishauri.

Mazoea yako hayo yametokana na kutokuwa na mpenzi na yanaweza kuathiri maisha yako ya mapenzi. Kama unahitaji mpenzi, itabidi uweke nia hiyo katika moyo wako kisha uchukue hatua.

Ameapa kuacha tabia zake chwara, siamini

Shangazi. Nilimuacha mpenzi wangu miezi miwili iliyopita kwa sababu ya mienendo yake isiyofaa. Sasa ameanza kunitafuta turudiane akisema ameacha tabia hiyo. Nishauri.

Uamuzi wako kuhusu ombi la aliyekuwa mpenzi wako utategemea tabia iliyokufanya umuache na jinsi unavyompenda. Kama amekwambia ameacha njia zake mbaya, mpe nafasi uone kama ni kweli.