Habari

Handisheki imesaidia kuleta amani, lakini isiue demokrasia – Washiali

September 26th, 2019 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA  [email protected] na DANIEL OGETTA  [email protected]

KUNDI la wabunge wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wanataka wanasiasa wa ODM kukoma kutumia ‘handisheki’ kuhujumu demokrasia nchini.

Wa hivi punde kusema hivyo ni kiranja wa wengi bungeni, Bw Benjamin Washiali ambaye kulingana naye, handisheki imeleta umoja katika serikali hivyo basi haifai kutumiwa kuhatarisha nafasi za chama kingine kushiriki kwenye kampeni za uchaguzi.

Kusudi la handisheki baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Bw Raila Odinga kulingana na Bw Washiali ni amani bali si kuhujumu chama kingine kiasi kwamba kinashindwa kushiriki kampeni za uchaguzi.

Tangu Rais Kenyatta kuunga uteuzi wa Mariga kupeperusha bendera ya Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra – ngome inayoaminika kuwa ya ODM- kumekuwepo na manong’enezi kuwa umoja uliopo kati ya viongozi hao unasambaratika.

Akizungumza Mumias, mbunge huyu wa Mumias Mashariki alitetea uteuzi wa mwanasoka McDonald Mariga kama mgombea katika uchaguzi mdogo wa Kibra.

“Tunaunga mkono handisheki kwa sababu imeleta amani nchini na kwamba haifai kutafsiriwa vibaya,” akasema Washiali.

Alieleza kwamba siasa za uchaguzi mdogo wa Kibra zinanuia tu kupata mwakilisha wa wakazi wa eneo hilo katika bunge na kwa namna oyote, hailengi kuhujumu handisheki.

“Mbona mnaipa Jubilee lawama kwa uteuzi wa mgombea katika uchaguzi mdogo wa Kibra, lakini Wiper licha ya kuwa katika memoranda ya maelewano na ODM, wamemteua mgombea?” alishangaa Washiali.

Kumpiga jeki

Aliongeza kwamba watampa Mariga msaada atakao kumwezesha kushinda katika uchaguzi huo.

Tangu kubuniwa kwa eneobunge hilo mnamo 2013, mwendazake Ken Okoth ndiye amekuwa mbunge. Alopoaga basi kikawa wazi, bila mwakilishi kwenye bunge.

Wabunge wa ODM nao wanaonelea kwamba Kibra ni ngome ya ODM kwani hata ilipokuwa katika eneobunge la Lang’ata, liliwakilishwa na Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa upinzani.

Katika uchaguzi ndogo za Embakasi Kusini na Ugenya mnamo Aprili, chama cha Jubilee hakikuteua mgombea.

Katibu mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna naye anadai kwamba vyama vya ANC na Jubilee kwa kuteua wagombea katika uchaguzi huu, vinasambaratisha mpango za handisheki

Imran Okoth ndiye anapeperusha bendera ya ODM, aliyekuwa mwandani wa Raila, Eliud Owalo akipeperusha bendera ya ANC nacho Ford Kenya kikimtegemea Khamisi Butichi kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi huo unaotarajiwa Novemba.

Japo ANC pia imejibwaga kwenye kinyang’anyiro, uchaguzi mdogo wa KIbra unaonekana kuleta joto baina ya  Naibu Rais William Ruto na Bw Odinga ambao ni vigogo wasiopatana tangu maelewano baina yao kusambaratika mnamo 2013.