Habari MsetoSiasa

Handisheki itamfikisha Raila Ikulu – ODM

March 25th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

CHAMA cha ODM kimekiri kuwa muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga utakirahisishia juhudi zake za kushinda urais ifikapo mwaka wa 2022.

Tangu muafaka huo ulipobuniwa mnamo Machi 9, 2018, Naibu Rais William Ruto na wandani wake wamekuwa wakilalamika kuwa ni njama ya ODM kumvurugia mipango yake ya kumrithi Rais Kenyatta.

Lakini Bw Odinga husisitiza kuwa nia yake katika handisheki ni kutimiza maazimio yatakayoleta umoja wa kitaifa na maendeleo nchini, ikiwemo kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.

Jumapili, Gavana wa Kakamega aliye pia Naibu Mwenyekiti wa ODM, Bw Wycliffe Oparanya alisema chama hicho kina mikakati kabambe kuhusu uchaguzi wa urais ujao na handsheki ni “njia ya mkato” kufika Ikuluni.

Alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wa wajumbe watakaowakilisha ODM katika uchaguzi mdogo wa ubunge eneo la Ugenya na kumpigia debe mgombeaji wao, Bw Chris Karani.

“Itakuwa aibu kubwa hiki kiti kikienda kwingine kwa sababu sisi kama chama tayari tumeanza kujitayarisha kwa 2022. Wale wanapanga na sisi tunapanga,” akasema.

Aliongeza: “Mnajua Baba alianza safari kuenda Canaan na sisi hatujafika Canaan. Saa hii tumefanya njia ya mkato kupitia kwa handisheki na sasa tuko karibu kabisa. Hatutaki kama tuko karibu mtu yeyote aharibu hii safari yetu.”

Alikuwa ameandamana na viongozi wengine wakiwemo maseneta James Orengo (Siaya), Cleophas Malala (Kakamega), Mwakilishi wa Kike wa Busia, Bi Florence Mutua na Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna.

Bw Orengo ambaye alizungumza kabla ya gavana huyo, alisisitiza ODM itakuwa kwenye debe 2022 na watu wasiwe na wasiwasi kuhusu atakayepeperusha bendera ya chama hicho.

“Sisi katika ODM tumejipanga. Vyama vingine havina mpango. Wengine wanajiuliza ikifika 2022 mambo yatakuwaje. Watu wanauliza kama Raila hasimami nani atasimama. Tunajua vile tumejipanga,” akasema.

Viongozi hao waliomba wapigakura wasimwaibishe Bw Odinga kwenye uchaguzi huo mdogo, wakidai utakuwa mashindano kati ya wanaounga mkono handsheki na wale wanaoegemea upande wa Dkt Ruto.

Wandani wa Naibu Rais ambao walizungumza wakiwa mtaa wa Mwiki, Kaunti ya Nairobi walizidi kusisitiza kuwa viongozi wa upinzani wana njama ya kuvuruga mipango ya Jubilee wakilenga siasa za 2022.