Habari MsetoSiasa

HANDISHEKI: Kisumu kupata taa za trafiki miaka 118 baadaye!

May 22nd, 2019 1 min read

Na JUSTUS OCHIENG

KISUMU itapata taa za trafiki kwa mara ya kwanza kabisa, miaka 118 tangu jiji hilo la eneo la Nyanza kujengwa, ishara ya matunda ya handisheki kuzidi kuenea katika ngome za kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Taa hizo zitatumika kudhibiti msongamano wa magari katika miungano ya barabara na vivuko vya wanaotembea kwa miguu.

Aidha, taa hizo za trafiki zitawekwa miaka 18 tangu rais mstaafu Daniel Arap Moi kutangaza rasmi Kisumu kuwa mji.

Mnamo 2001, Kisumu iliadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake katika sherehe ya kufana iliyohudhuriwa na marais Daniel Moi, Yoweri Museveni wa Uganda na mstaafu Benjamin Mkapa wa Tanzania.

Ni katika maadhimisho hayo ambapo Moi alitangaza Kisumu kuwa mji.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Barabara Kuu (KeNHA) Bw Peter Mundinia, alisema jana kuwa taa hizo zitawekwa katika miungano mitatu mikuu kwenye barabara ya Kisumu-Kakamega.

Bw Mundinia alisema kando na kuimarisha miundomsingi na kujenga barabara hiyo kuu ili iwe ya pande mbili, kumekuwa na haja ya kuweka taa za trafiki ili kuleta usalama barabarani kwani hii itasaidia kupunguza ajali.

Alieleza: “Kuna vivuko vya wanaotembea kwa miguu na pia miungano ya magari kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine, hivyo taa zitahakikisha miundomsingi hii inatumika vyema zaidi.”

Mkurugenzi huyo alisema kampuni ya NAS International ndiyo imegawiwa kandarasi ya kuweka taa hizo kutoka kwa kampuni ya SBI International Holdings ambayo ndiyo inajenga barabara ya pande mbili ya Kisumu-Nyang’ori.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NAS Bw Nicholas Airo alisema taa hizo za trafiki zitawekwa katika mizunguko ya Kisumu Boys, Patels na Kondele.

“Tayari tumeanza kuweka taa Patels na tutaendelea katika miungano hiyo mingine,” Bw Airo aliambia Taifa Leo.

Aliongeza kuwa watafanya hamasisho kwa umma na shuleni kwa wanafunzi pamoja na kukutana na wadau wote wa uchukuzi ili kuwahamasisha kuhusu matumizi ya taa za trafiki.