Habari

Handisheki kufa baada ya refarenda

November 30th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, amesema kwamba, ukuruba wake na Rais Uhuru Kenyatta utafikia kikomo baada ya kura ya maamuzi wanayoandaa kupitia mchakato wa maridhiano (BBI).

Waliposalimiana Machi 9, 2018, kulikuwa na wasiwasi kwamba, huenda viongozi hao wawili walikuwa na mipango ya kubadilisha katiba ili kuwawezesha kudhibiti siasa na utawala Kenya, ilivyofanyika Urusi kati ya Rais Vladimir Putin na Dmitry Medvedev.

Kati ya 2008 na 2012, Putin alipokabiliwa na kizingiti cha kikatiba kugombea kwa kipindi cha tatu cha urais, alikubaliana na Medvedev akachukua wadhifa wa uwaziri mkuu ambao sio wa hadhi kama urais na wakaendelea kutawala. Mnamo 2012, alichaguliwa rais naye Medvedev akawa waziri mkuu.

Licha ya Rais Uhuru na Bw Odinga kusisitiza kuwa muafaka wao haukuhusu siasa za urithi mwaka wa 2022 Rais Kenyatta anapotarajiwa kuondoka mamlakani, kulikuwa na hofu kuwa Rais Kenyatta alikubaliana na Bw Odinga amuunge mkono kuwa mrithi wake ili amteue waziri mkuu.

Mnamo Jumamosi, Bw Odinga aliwaondolea wasiwasi wafuasi wake kwa kusema kwamba handisheki yake na Rais Kenyatta itafikia kikomo baada ya kura ya maamuzi wanayoendelea kuandaa.

“Tunaelekea mwisho wake (handisheki). Serikali ya sasa itaondoka ofisini 2022,” alisema alipoulizwa iwapo alihofia kwamba Rais Kenyatta angemcheza shere.

Ikizingatiwa kwamba mkataba wao ulikuwa wa siri na haukulindwa kisheria, baadhi ya wandani wa Bw Odinga walihisi kwamba Rais Kenyatta alitumia handisheki kutuliza joto la kisiasa kwa kufifisha upinzani kisha amteme kipindi chake cha uongozi kikikaribia kukamilika.

“Uliona Rais akisimama kidete kusema kwamba tutafanya kura ya maamuzi. Referenda ikifanyika, tutakuwa tumemalizana,” Bw Odinga alisema mnamo Jumamosi kwenye mahojiano na gazeti Sunday Nation.

Bw Odinga alisema hatua ambazo yeye na Rais Kenyatta wamepiga katika mipango yao ya kubadilisha katiba, hakuna anayeweza kusaliti mwingine.

“Swali la rais au mimi kujiondoa katika mkataba wetu limepitwa na wakati. Sasa tumefikia awamu ya kura ya maamuzi na tunaweza tu kuzungumzia maswala mengine tukifaulu au kushindwa,” Bw Odinga alisema.

Kauli yake na ya Rais Kenyatta kwamba atastaafu 2022 imeondoa wasiwasi kwamba lengo lao ya kubadilisha katiba kubuni nyadhifa za waziri mkuu lilinuiwa kuwawezesha kushirikiana kuongoza nchi.

Baadhi ya waliokosoa handisheki yao na mchakato wa kubadilisha katiba, walikuwa wakidai Rais Kenyatta alitaka kumsaidia Bw Odinga kuingia mamlakani ili amteue waziri mkuu.

Wasiwasi huo uliongezeka mnamo Novemba 2019, Rais Kenyatta aliponukuliwa akisema hatajali kuwa waziri mkuu katiba ikifanyiwa mageuzi.

“Nasikia watu wakidai kwamba Uhuru Kenyatta anataka kuwa waziri mkuu wa Kenya. Siwezi kukataa kuongoza katika wadhifa huo lakini tushughulikie hali inayotukabili sasa,” Rais Kenyatta alisema alipokutana na viongozi wa eneo la Mlima Kenya mjini Nyeri 2019.

Baadhi ya wandani wake akiwemo naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe na katibu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu) pia waliendeleza mdahalo huo wakidai angali na umri mdogo kustaafu siasa.

Hata hivyo, kuanzia Januari mwaka huu Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa lengo lake kuunga marekebisho ya katiba sio kutaka kukwamilia mamlakani bali kuunganisha Wakenya wasiwe wakipigana kila baada ya uchaguzi.

Kulingana na wataalamu wa katiba, mchakato wa kubadilisha katiba wa BBI ambao viongozi hao wanaongoza, itabidi Rais Kenyatta agombee ubunge kwanza kuweza kuteuliwa waziri mkuu hatua ambayo itakuwa ni kujishusha hadhi.