Habari MsetoSiasa

Handsheki: Wakazi wajuta kurushia Uhuru kiatu 2014

January 20th, 2020 2 min read

Na IAN BYRON

BAADHI ya wakazi katika Kaunti ya Migori wamejutia kisa ambapo Rais Uhuru Kenyatta alirushiwa kiatu jukwaani miaka sita iliyopita, wakishuku kisa hicho kimefanya wakose matunda ya handsheki.

Huku maeneo mengine ya Nyanza na ngome za kisiasa za Kiongozi wa ODM Raila Odinga kitaifa zikiendelea kupokea maendeleo tangu handsheki yake na Rais, wakazi hao wamesema miradi imekwama katika eneobunge la Suna Mashariki.

Kulingana nao, tukio hilo la aibu lililoshuhudiwa mnamo Septemba 8, 2014 huenda lilifanya wakaorodheshwa kama maadui wakubwa wa serikali ya Jubilee.

Kiatu kilirushwa jukwaani wakati Rais Kenyatta alipokuwa ameenda kuzindua ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Kakrao na uwekaji lami barabara ya Migori kuelekea Muhuru.

Miaka sita baadaye, hata miradi hiyo iliyoenda kuzinduliwa haijaguswa.

Wakiongozwa na kiongozi wa vijana Migori, Bw Joseph Nyapete, wakazi hao walisema hawajaona dalili yoyote kwamba handsheki itawaokoa ili wafurahie maendeleo kutoka serikalini.

Taasisi ya Kakrao iliyonuiwa kuwa jengo la orofa tatu ilikwama wakati orofa ya chini ilikuwa inajengwa na sasa uwanja umejaa vichaka huku vifaa vya ujenzi vikiporwa.

“Mahali hapo panatisha. Ni aibu kwa handsheki kwani ni eneobunge la Bw Junet Mohamed ambaye yuko mstari wa mbele kutetea handsheki,” akasema Bw Nyapete.

Mzee Samuel Migore ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema ukarabati wa barabara ya Migori-Muhuru ilikwama katika eneo la Masara, kisha mradi ukaelekezwa mjini Kehancha ambako ni ngome ya Jubilee.

“Hakuna vile tunaweza kuzungumzia matunda ya handsheki wakati miradi hii imekwama,” akasema Bw Migore.

Ijapokuwa kisa hicho kilitokana na uhasama kati ya Gavana wa Migori Okoth Obado na baadhi ya wabunge katika kaunti hiyo, wakazi wanasema wananchi ndio wanaumia kutokana na athari zake.

Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Rongo, Prof Gudu Samuel Gudu alitoa wito kwa Bw Junet na Gavana Obado kutoa ufadhili wa kukamilisha ujenzi wa taasisi ya Kakrao. Taasisi hiyo inastahili kusimamiwa na Chuo Kikuu cha Rongo.

Bw Charles Ochieng’ Ogejo, ambaye ni msaidizi wa kibinafsi wa Bw Junet alisema Hazina ya Ustawishaji Maeneobunge ya Suna Mashariki tayari ilitenga Sh10 milioni, lakini juhudi za afisi ya eneobunge zikavurugwa na serikali ya kaunti.