HabariSiasa

Hapa hujuma tu!

February 26th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MABILIONI ya pesa za umma yameharibiwa kwenye miradi mikubwa ya Serikali ya Jubilee, ambayo imekwama au imeshindwa kuwa ya manufaa kwa umma.

Mradi wa hivi majuzi kupata pigo ni wa vipakatalishi kwa watoto wa darasa la kwanza, ambao ulivumishwa vikali na wakereketwa wa Jubilee walipoingia madarakani 2013.

Hii ni baada ya Wizara ya Elimu kusema imebadilisha sera kuhusu mradi huo, na kwa hivyo itakoma kuwapa watoto laptopu hizo.

Badala yake, alisema Katibu wa Wizara ya Elimu, Belio Kipsang, watajenga maabara za tekinolojia katika shule zote 25,000 za umma nchini.

“Sera imebadilika kutoka kumpa kila mwanafunzi kipakatalishi, na sasa itakuwa ni ujenzi wa maabara ya kompyuta kwa mafunzo ya ICT,” alinukuliwa.

Kulingana na Ripoti ya Wizara ya Elimu mnamo Desemba mwaka 2018, mafanikio ya mradi huo ni asilimia tano pekee. Hii ni licha ya Sh42.3 bilioni kutumika katika mradi huo.

Haya yalitokea siku chache baada ya kugunduliwa kwamba mradi mkubwa wa unyunyizaji maji katika shamba la Galana Kulalu, Kaunti ya Tana River pia umekwama, baada ya serikali kutumia Sh5.9 bilioni kulipa kampuni ya Israeli iliyokuwa ikijenga miundomsingi katika shamba hilo.

Mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa alisema wabunge wataitisha ripoti kutoka kwa serikali ili ifafanuliwe jinsi fedha zilizotengewa miradi hiyo.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo kuhusu vipakatalishi, Bw Wamalwa alisema: “Tulisema wazi tulipokuwa katika Muungano wa Cord na NASA kwamba mpango huo ulibuniwa bila nia ya kusaidia wananchi, bali kujaza pesa mifuko ya watu wachache. Tunataka uwajibikaji kuhusu jinsi fedha zilivyotumiwa.”

Ripoti zilisema kampuni iliyohusika katika Galana iliondoka kabla ya kukamilisha ujenzi wa miundomsingi kwani haikuwa imelipwa pesa zote.

Kwa upande wake, Bodi ya Kitaifa ya Unyunyizaji (NIB) ilidai kampuni hiyo ya Green Arava, ilikiuka makubaliano na haikutekeleza kazi kama ilivyotarajiwa.

Utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulikuwa umenuia kutumia mradi huu kama mfano wa mbinu za kisasa za kilimo zitakazofanikisha uzalishaji wa chakula kitakachotosheleza mahitaji ya umma.

Awali, Wizara ya Elimu nayo ilimulikwa kwa madai ya ubadhirifu wa fedha katika usambazaji wa vitabu vya kusoma kwa shule za umma, huku ikihofiwa karibu Sh10 bilioni zilifujwa.

Mradi mwingine mkuu ambao Rais alitumaini kuutumia kuacha sifa bora kabla aondoke mamlakani 2022, ni wa usambazaji wa maji safi kwa wananchi kupitia ujenzi wa mabwawa katika sehemu mbalimbali za nchi.

Lakini hili pia linaonekana kukumbwa na dhoruba kali kwani imebainika kuwa kampuni iliyopewa zabuni ya ujenzi wa mabwawa matano maeneo ya Rift Valley na Kaunti ya Meru kwa gharama ya Sh104.5 bilioni haina uwezo wa kutekeleza ujenzi huo.

Jana, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliagiza wakurugenzi wa kampuni 107 zinazoaminika zilihusika katika ufujaji wa fedha katika ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, wafike katika idara hiyo ili kusaidia katika uchunguzi ulioanzishwa.

Mradi mwingine ambao umekwama ni utoaji wa mbegu na fatalaiza kwa bei nafuu, ambao Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri tayari amesema hautatekelezwa mwaka huu kutokana na ukosefu wa ufadhili. Hii ni licha ya kuwa ulitengewa pesa kwenye bajeti ya 2018/2019.

Tangu ulipoanzishwa mnamo 2014, jumla ya Sh19.3 bilioni zimetumika kwa ununuzi wa mbegu na mbolea za bei nafuu.

Hata hivyo, mradi huo umekuwa ukikumbwa na madai ya ulaghai wa mbolea na mbegu mbovu, pamoja na maafisa kuuza fatalaiza hiyo kwa wafanyibiashara, ambao baadaye wanawauzia wakulima kwa bei ya juu.

Kwa upande mwingine, lengo kuu la kusaidia vijana kubuni nafasi za kazi kupitia kwa Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) na Hazina ya Vijana (YEF) imetatizika kutokana na wizi wa pesa katika mashirika hayo.