Michezo

HAPA KITANUKA: Patachimbika Barca, Reds wakionana

April 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LISBON, Ureno

BAADA ya kuibandua nje FC Porto kwenye hatua ya robo-fainali, Liverpool ina mlima mrefu wa kupanda itakapokutana na FC Barcelona ya Lionel Messi katika nusu-fainali ya dimba la Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA).

Vijana hao wa kocha Jurgen Klopp waliandikisha ushindi mkubwa wa mabao 4-1 dhidi ya Porto ugenini, Jumatano usiku na sasa wanajiandaa kuvaana na vijana wa Ernesto Valverde kuwania nafasi ya kutinga fainali.

Staa wao matata Sadio Mane alipachika wavuni bao la kwanza ambalo baada ya ubishi, ilibidi uamuzi utolewe na mtambo wa VAR.

Mshambulizi wa Liverpool, Sadio Mane (kati) asherehekea na wenzake baada ya kufunga bao kwenye robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Porto ugani Dragao mjini Porto, Ureno mnamo Jumatano, Aprili 17, 2019. Picha/ AFP

Kulikuwa na madai kwamba raia huyo wa Senegal alikuwa ameotea, lakini mtambo huo ukaonyesha alikuwa tu kwa laini.

Liverpool waliingia uwanjani wakijivunia ushindi wa 2-0 walioupata ugani Anfield katika mkondo wa kwanza.

Mabao yao mengine yalipatikana kupitia kwa Mohamed Salah, Roberto Firmino na Virgil van Dijk, huku la Porto likifungwa na Eder Militao zikibakia dakika 21 mechi hiyo kumalizika.

Yalikuwa matokeo ya kuudhi kwa timu ya nyumbani ambayo mwezi Februari 2018 ilicharazwa 5-0 na vijana hao wa Klopp, pia uwanjani humo.

Kutokana na ushindi huo, Liverpool wataanzia ugenini dhidi ya Barcelona, hii ikiwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana tangu zikabiliane msimu wa 2006/07 katika hatua ya 16 bora, ambapo Liverpool ilishinda kutokana na bao la ugenini.

Ni ushindi ambao pia umehuisha matumaini yao ya kutwaa mataji mawili msimu huu- la EPL na UEFA.

Hii ilikuwa mechi yao ya 17 bila kushindwa na ya nane ya ushindi mfululizo, ingawa wanatarajia upinzani mkali kutoka kwa Barcelona ambao ni wakali zaidi kuliko Porto.

Ligi

Wakati mkondo wa kwanza ukisubiriwa, Liverpool itaelekeza macho yake kwa mechi za EPL ambako imepangiwa kucheza na Cardiff City na Huddersfield Town, kabla ya pambano hilo la UEFA.

Baadaye itakutana na Newcastle United na Wolves. Huku akitarajia kibarua kigumu katika mechi zijazo za nyumbani, kocha Klopp alifanya mabadiliko matano kikosini baada ya ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Chelsea.

Firmino na Naby Keita ambao walifunga kwenye mechi hiyo pamoja na Jordan Henderson waliingia katika nafasi za Georginio Wijnaldum, James Milner na Divock Origi.

Wakati huo huo, staa wa Liverpool, Mohamed Salah amesema iwapo watashinda mechi nne zilizobakia katika EPL, watashinda ligi kuu msimu huu.

Salah alifunga bao katika ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Chelsea na kufanya mbio za kuwania ubingwa huo kuwa ngumu zaidi kwa wapinzani wao wakuu, Manchester City.