Na BENSON MATHEKA
UCHAGUZI mkuu wa 2022 unapokaribia, vyama vikuu vya kisiasa vinaendelea kudhihirisha kiwango cha juu cha udikteta unaoweza kuvisambaratisha huku vinara wake wakiadhibu wanachama wanaohisi kuwa vikwazo kwa azma zao.
Hali hii imeshuhudiwa hasa wakati huu nchi inapojiandaa kwa kura ya maamuzi ambayo viongozi wa vyama vya kisiasa wanaunga ili kutimiza maslahi yao ya kisiasa.
Tangu mchakato huo uanze, demokrasia imefifia katika vyama vya kisiasa vinavyodai kuwa vinaitetea. Katika chama cha ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga anayetambuliwa kuwa baba wa demokrasia nchini, wanaoibua maswali kuhusu mchakato huo wanachukuliwa kuwa mahasimu na wasaliti, kukemewa na kuadhibiwa.
Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, alipokonywa wadhifa wa Naibu mwenyekiti wa kamati ya Sheria ya Bunge (JLAC) kwa kukosoa msimamo wa chama kuhusu baadhi ya mapendekezo katika mswada wa BBI.
Kabla ya hatua hiyo, Bw Amollo na Seneta wa Siaya James Orengo walikuwa wameshutumiwa na baadhi ya viongozi wa ODM kwa kuhujumu mipango ya Bw Odinga katika BBI.
Kwa haya kutokea katika chama ambacho kinadai kwamba kinakumbatia demokrasia, ni ishara kuwa viongozi wake, wameamua kuirusha kwenye dirisha ili kulinda maslahi ya Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
“Inasikitisha kwamba chama ambacho kimekuwa kikidai kuwa mhimili mkubwa wa demokrasia nchini na kinachoongozwa na baba wa demokrasia kinaweza kutumbukia katika udikteta kama ulioshuhudiwa chama cha Kanu na ambao Bw Odinga amekuwa akipinga kwa miaka mingi,” asema mchanganuzi wa siasa Richard Kigen.
Mchanganuzi huyu anasema japo kwa miaka mingi vyama vya kisiasa nchini Kenya ni mali ya vigogo wa kisiasa, yanayoshuhudiwa kwa wakati huu wa mchakato wa kura ya maamuzi ni kilele cha udikteta.
“Tangu handisheki, mambo yalibadilika huku wanaotofautiana na vinara wa vyama vyao wakitishiwa, kutengwa na kupokonywa nyadhifa za uongozi katika bunge na vyama. Hii inaweka vyama hivi katika hali hatari uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia,” asema Kigen.
Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye ni naibu kiongozi wa ODM anahofia kwamba refenda ya BBI itasambaratisha chama hicho cha chungwa.
Chama cha Jubilee kimegawanyika kati ya mirengo ya Kieleweke unaojumuisha wabunge wanaomuunga Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa chama hicho na Tangatanga wa wabunge wanaomuunga Naibu Rais William Ruto ambaye ni naibu kiongozi wa chama.
Kwa sababu ya kukosoa handisheki, Dkt Ruto na washirika wake wametengwa serikalini na chamani na dalili zinaonyesha ifikapo 2022, Jubilee kitakuwa kimefifia tofauti na kilivyokuwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
“ Hii ni kwa sababu ya udikteta uliozuka katika chama baada ya watu wawili kusalimiana na kufanya maamuzi yanayolenga kutimiza maslahi ya watu binafsi badala ya Wakenya wote,” asema mbunge mmoja wa chama hicho ambaye aliomba tusitaje jina lake.
“Vitisho na maamuzi ya mtu mmoja ni hatari. Mfumo wa kidemokrasia tulioweka katika Jubilee ulisambaratishwa na nafasi yake kuchukuliwa na mfumo wa kiimla,” alisema aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando.
Wabunge wanaomuunga Dkt Ruto wamevuliwa nyadhifa katika chama hicho na bungeni. Baadhi yao ni Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata ambaye alipokonywa wadhifa wa kiranja wa wengi katika seneti kwa kuandikia Rais Kenyatta barua akimweleza kwamba BBI sio maarufu eneo la Mlima Kenya.
Katika chama cha Wiper, uamuzi wa kiongozi wake Kalonzo Musyoka wa kuunga BBI ulisababisha mgawanyiko uliofanya aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana kukihama. Wawili hao walimlaumu kwa kufanya maamuzi uq kidikteta.
Kuhama kwa wawili hao ambao kunaweza kufifisha umaarufu wa chama hicho eneo la Ukambani kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Kulingana na Bw Kibwana, chama cha Wiper kinasimamiwa kwa mabavu na uongozi wake haujali maslahi ya raia wa kawaida madai ambayo Bw Muthama anaunga.
“Singevumilia kuona Bw Musyoka akitelekeza jamii kwa uamuzi wake wa kushirikiana na Rais Kenyatta,” asema.
Mjadala wa mswada huo umegawanya chama hicho huku washirika wa karibu wa Bw Musyoka wakiwemo maseneta Enock Wambua wa Kitui na Mutula Junior wakimkaidi.
Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba udikteta wa viongozi wa vyama vikubwa vya kisiasa unazua mizozo inayoweza kuvisambaratisha.
Kwa mfano, ni wazi kuwa idadi kubwa ya wabunge wa Jubilee wanasubiri kujiunga na United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Dkt Ruto.
Baadhi ya wabunge wa ODM wanaweza kujiunga na chama cha People’s Democratic party cha Gavana Okoth Obado wa Migori. Tayari chama cha Maendeleo Chap Chap cha Gavana wa Machakos Alfred Mutua kinapatia Wiper ushindani mkubwa eneo la Ukambani,” asema Bw Kigen.