Habari

Harakisheni BBI – Mudavadi

December 14th, 2020 2 min read

PATRICK LANGAT Na CECIL ODONGO

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi alionekana kupiga abautani Jumapili na kushinikiza mchakato wa kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) uharakishwe.

Bw Mudavadi alisema Wakenya wameshiriki mjadala kuhusu mchakato huo kwa muda mrefu na unafaa kukamilishwa haraka ili washughulike na masuala mengine.

Bw Mudavadi alisema imechukua muda wa miaka miwili Wakenya na wanasiasa wakiunga ama kupinga ripoti hiyo na sasa umewadia wakati ambapo suala hilo linafaa limalizwe kabisa.

Alilinganisha BBI na jipu mwilini ambalo uhitaji kutobolewa ili kidonda kipone, akiashiria kuwa ripoti hiyo sasa ipo sawa na inahitaji kupitishwa ili taifa lizangatie masuala mengine.

“Tumekuwa tukizungumza kuhusu BBI kwa muda wa miaka miwili unusu. Ni suala ambalo hatuwezi kuendelea kulizungumzia milele. Tunafaa sasa kuondoa jipu hilo ili kidonda chenyewe kipone,” akasema Bw Mudavadi katika Kanisa la Friends mtaani Maringo, eneobunge la Makadara, Kaunti ya Nairobi wakati wa ibada ya Jumapili.

Makamu huyo wa Rais wa zamani alikuwa ameandamana na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, mbunge wa eneo hilo George Aladwa, Mwakilishi wadi wa Umoja 1 Mark Ndung’u na mwanasiasa Stanley Livondo.

Alifichua kwamba ameridhika na mabadiliko yaliyofanyiwa ripoti ya BBI akiahidi kuwa mmoja wa viongozi watakaoivumisha kwa kuwa ina manufaa mengi kwa Wakenya.

“Wakati ambapo ripoti ya pili ya BBI ilitolewa, kuna masuala ambayo hatukukubaliana kuyahusu ndipo tukasisitiza lazima kuwe na mabadiliko. Kwa sasa asilimia 80 ya masuala tuliyoyaibua yameshughulikiwa na tunataka tumalize kupitisha ripoti hiyo na kumakinikia uboreshaji wa uchumi wetu,” akaongeza Bw Mudavadi.

Wakati wa kuzinduliwa kwa ripoti ya BBI Oktoba 26, Bw Mudavadi alisema ripoti hiyo ilifaa kubadilishwa ili kulipa bunge la seneti nguvu, na pia akashikilia kwamba afisa wa kupokea malalamishi kuhusu mahakama anafaa ateuliwe na Jaji Mkuu wala si Rais.

Wakati huo pia alisisitiza kwamba, ripoti hiyo haikugusia jinsi serikali itapunguza deni kubwa ambalo nchi hii inadaiwa na mataifa ya kigeni.

Hata hivyo, alikuwa kati ya wanasiasa wakuu waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa ukusanyaji wa saini akisema masuala aliyoyaibua katika ukumbi wa Bomas yalitiliwa manani kwenye ripoti ya pili.

Ilibainika kuwa Bw Mudavadi alibadilisha nia kuhusu mchakato huo baada ya kukutana na Rais Kenyatta baada ya uzinduzi wa ripoti katika ukumbi wa Bomas.

Yeye ni miongoni mwa vigogo wa kisiasa wanaomezea mate nyadhifa za uongozi zitakazobuniwa katiba ikifanyiwa mageuzi.

Bw Sakaja naye alisifia kuondolewa kwa kipengele kwenye ripoti ya pili ya BBI kilichohamisha majukumu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi hadi kwa Shirika la Huduma kwa Wakazi wa Jiji (NMS).

“Tumesisitiza kwamba huwezi kutatua tatizo la muda kupitia suluhu ya milele. Tunataka Nairobi inufaikie ma ugatuzi kama kaunti nyingine 47. Tunafuraha kwamba kilio chetu kilisikizwa na hata tukaongezwa maeneobunge mengine 12. Hilo litahakikisha uwakilishi wa raia upo sawa na huduma zinawafikia kwa urahisi,” akasema Bw Sakaja