Michezo

Harambee Starlets jicho Tokyo wakialika Shepolopolo leo Ijumaa

November 8th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

TIMU ya taifa ya Harambee Starlets leo Ijumaa itajibwaga uwanjani Kasarani kuvaana na timu ya taifa ya Zambia katika mechi ya kuwania nafasi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2020 nchini Japan.

Mechi ya marudiano imeratibiwa kuchezewa jijini Lusaka, Zambia, Jumanne ambapo mshindi atakutana na Ivory Coast au Cameroon katika raundi ya mwisho ya kuwania tiketi hiyo ya kwenda Tokyo.

Timu itakayoshindwa itakutana na Chile katika mchujo wa kuwania nafasi ya kwenda Tokyo.

Akizungumza kuhusu pambano hilo, kocha David Ouma alisema kikosi kipo tayari kupigania ushindi.

Kikosi cha Zambai maarufu kama Shepolopolo kiliwasili nchini Jumatano kwa mechi hiyo itakayoanza saa kumi.

Starlets wamekuwa kambini tangu Alhamisi iliyopita, baada ya kuibandua Ghana katika raundi iliyopita.

Chile ilimaliza ya pili katika fainali za bara la Amerika Kusini (Conmebol).

Wakati huo huo, mshambuliaji wa timu ya taifa ya Harambee Starlets, Teresa Engesha amesema yuko katika hali nzuri ya kupigania taji la mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kandanda ya Wanawake nchini (KWPL) msimu huu.

Engesha ambaye ni mshambuliaji matata wa klabu ya Vihiga Queens FC ya Alex Alumira aliachwa nje ya kikosi cha sasa cha Starlets chini ya David Ouma katika mchujo wa mwisho wa kuunda timu hiyo.

Katika pambano la ligi, Engesha kwa sasa yuko kileleni mwa jedwali la wafungaji bora baada ya kupachika wavuni mabao 35 katika mechi za 26 kikosi hicho.

Katika mahojiano mjini Mbale mnamo Jumatano, Engesha alisema yuko katika mazoezi ya hali ya juu ambayo yananuia kumwezesha kutimiza azma hiyo yake.

Makipa ni: Annette Kundu (Eldoret Falcons), Judith Osimbo (Gaspo Women), Wilfrida Seda (Vihiga Queens), Monica Odato (Wadadia)

Walinzi: Vivian Nasaka (Vihiga Queens), Dorcas Shikobe (Oserian Ladies), Lydia Akoth (Thika Queens), Lucy Akoth (Mathare United Women), Ruth Ingosi (Eldoret Falcons), Wincate Kaari (Gaspo Women), Nelly Sawe (Thika Queens), Dorcas Shiveka (Eldoret Falcons) na Sylvia Lumasia (Kibera Girls Soccer Academy)

Viungo: Jentrix Shikangwa (Wiyeta Girls), Cynthia Shilwatso (Vihiga Queens), Sheril Angachi (Gaspo Women), Corazone Aquino (Gaspo Women), Mwanalima Adam (Thika Queens), Elizabeth Wambui (Gaspo Women) na Providence Kasiala (Wiyeta Girls).

Washambuliaji: Topistar Situma (Vihiga Queens), Bertha Omita (Kisumu All Starlets), Mercy Airo (Kisumu All Starlets) na Janet Bundi (Eldoret Falcons).