Michezo

Harambee starlets watiwa adabu na Crested Cranes

July 19th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MIAMBA Harambee Starlets wameanza kampeni yake ya kutafuta taji la Soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kulimwa 1-0 na limbukeni Crested Cranes ya Uganda katika mechi ya ufunguzi uwanjani Nyamirambo jijini Kigali, Rwanda, Alhamisi.

Starlets ya kocha David Ouma, ambayo ilizaba Uganda 1-0 Aprili katika mechi ya raundi ya kwanza ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika baadaye mwaka huu wa 2018 kabla ya kupigwa breki na Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 3-2 Juni, ilizamishwa na bao la Lilian Mutuuzo. Mganda huyu alimwaga kipa Poline Atieno katika dakika ya saba.

Mkenya Mwanahalima Adam almaarufu Dogo alipata nafasi nzuri dakika ya 20, lakini shuti lake likagonga mwamba.

Kenya iliendelea kushambulia na hata kudhani imepata bao la kusawazisha pale Neddy Atieno alipotikisa nyavu dakika ya 38, lakini halikusimama kwa sababu alikuwa ameotea. Dakika mbili baadaye, Teresa Engesha alikosa nafasi ya wazi aliposalia pekee yake na kipa Ruth Aturo, lakini akapiga nje.

Ouma alifanya mabadiliko mawili dakika ya 57 akiwaingiza washambuliaji Esse Akida na nyota wa timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 Martha Amunyolete katika nafasi za Mercy Achieng’ na Teresa Engesha.

Akida, ambaye alikuwa mfungaji bora katika makala yaliyopita mwaka 2016 alipocheka na nyavu mara sita, alijaribu kila mbinu kuokoa chombo kisizame bila mafanikio. Neddy alijaza wavuni bao dakika ya 77, lakini pia alipatikana ameotea.

Kenya na Uganda zinaorodheshwa katika nafasi za 123 na 131 mtawalia kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Starlets ilifika fainali ya mwaka 2016 ikiwa ni pamoja na kunyuka Uganda 4-0 katika mechi za makundi. Ilizabwa 2-1 na Tanzania katika fainali. Makala ya mwaka 2018 yamevutia Kenya, Uganda, Tanzania, Ethiopia na wenyeji Rwanda. Inatumia mfumo wa mzunguko.

Vikosi vya Kenya na Uganda (wachezaji 11 wa kwanza):

Kenya – Poline Atieno (kipa), Lilian Adera, Dorcas Shikobe, Elizabeth Ambogo, Wendy Achieng (nahodha), Cheris Avilia, Cynthia Shilwatso, Mercy Achieng, Mwanahalima Adam, Neddy Atieno, Terry Engesha. 

Uganda – Ruth Aturo (kipa), Viola Namuddu, Grace Aluka, Shadia Nankya, Yudaya Nakayenze, Tracy Jones Akiror(nahodha), Lilian Mutuuzo, Phiona Nabbumba, Ziana Namuleme, Juliet Nalukenge, Norah Alupo.