Michezo

Harambee Starlets yaipiga Northern Ireland mabao 2-0

March 5th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Kenya walitangaza kuwasili kwao katika mashindano ya kimataifa ya Turkish Women’s Cup kwa kishindo baada ya kulipua Northern Ireland Under-19 kwa mabao 2-0 mjini Alanya, Uturuki, Jumatano usiku.

Harambee Starlets ilifungua ukurasa wa mabao dakika ya 62 kupitia kwa kiungo Janet Bundi baada ya kutokea msongamano kwenye lango la Northern Ireland uwanjani Gold City Sport Complex.

Kiungo Jentrix Shikangwa, ambaye mwezi Januari aliibuka chipukizi bora kwenye tuzo za kitaifa za Kenya (SOYA), aliongeza bao la pili dakika ya 75 alipopokea krosi safi kutoka kwa mshambuliaji Mwanahalima “Dogo” Adam na kukamilisha kwa ustadi kupitia kichwa chake.

Warembo wa kocha David Ouma, ambao wamealikwa kushiriki makala hayo ya tatu kwa mara yao ya kwanza kabisa, wanashikilia nafasi ya pili katika Kundi B kwa tofauti ya ubora wa magoli na Chile waliopepeta Black Queens kutoka Ghana 3-0.

Wachile pia walipata magoli yao katika kipindi cha pili kupitia kwa Karen Araya (penalti), Camila Saez na Daniela Pardo.

Starlets itarejea uwanjani mnamo Machi 7 kuchapana na Chile katika mechi yake ya pili mjini Antalya. Ghana na Northern Ireland zitakabana koo katika mechi yao ya pili siku iyo hiyo mjini Alanya.

Kenya inatumia kombe hilo kujitayarisha kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AWCON) 2020 zitakazoanza mwezi Aprili. Starlets itaanza kampeni yake dhidi ya Tanzania katika raundi ya kwanza. Ikishinda Tanzania, itamenyana na mshindi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sao Tome & Principe katika raundi ya pili ambayo mshindi atafuzu kushiriki AWCON baadaye mwaka 2020.

Turkish Women’s Cup linashirikisha timu nane. Kundi A linaongozwa na Romania iliyochabanga Hong Kong 4-1 nayo Hungary ni ya pili baada ya kuzaba klabu ya BIIK Kazygurt kutoka Kazakhstan 2-1.