Michezo

HARAMBEE STARS: Francis Kimanzi ataweza?

August 17th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

KOCHA mpya wa Harambee Stars, Francis Kimanzi bila shaka amejiweka katika mkondo mkali wa kitaaluma katika majukumu yake ya sasa kama mkufunzi wa Harambee Stars.

Kwa kocha huyu ambaye alizaliwa katika Kaunti ya Kitui mnamo Mei 29, 1976, na akajipa malezi ya wazazi katika mtaa wa Mlango Kubwa jijini Nairobi, kuchukua mikoba ya Harambee Stars kwa sasa, pengine ni kazi kubwa na ngumu kwake ikizingatiwa kuwa amekuwa akiipata na kuipoteza mara si moja.

Anaingia wakati ambapo mashabiki wangali na hisia mbaya kufuatia kichapo katika dimba la Afcon 2019 ambapo nchini Misri, Harambee Stars ilipoteza mechi mbili – dhidi ya Algeria na Senegal – kati ya tatu na kung’atuka mapema katika awamu ya makundi.

Kenya ilishinda Tanzania.

Ingawa hivyo, matumaini ni kuwa Kimanzi anatarajiwa kurekebisha hali.

Muhimu ni kwamba ana kibarua ikizingatiwa kuwa droo ya awamu ya mechi za kufuzu Afcon 2021 katika taifa la Cameroon imetoka na ambapo atazipiga dhidi ya Misiri, Visiwa vya Comoros na Togo.

Kimanzi hafichi pingamizi zake kwa makocha wa kigeni na kwa sasa amerithi mikoba hiyo ya harambee Stars kutoka kwa Mfaransa Sebastian Migne na kujitakasa, ni afanye vyema kumliko mtangulizi huyo ambaye alifufua matumaini ya kuweka Kenya katika rada pana ya kimichezo kwa kufanikisha Stars kutua Misiri.

Mzozo wa kikazi

Kati ya 1994 na 2002 Kimanzi alikuwa akiwajibikia usogora ugani kwa timu ya Mathare United na mnamo Desemba 1, 2008, akawajibishwa mikoba ya Stars kwa mara ya kwanza.

Alipigwa kalamu Januari 2009 baada ya kuingia kwa mzozo wa kikazi na wasimamizi wa kandanda nchini.

Alitua katika ukufunzi wa timu ya Ligi kuu ya taifa ya Sofapaka “Batoto ba Mungu” kwa mwaka mmoja na akateuliwa tena kuwajibikia ukufunzi wa Harambee Stars mnamo Novemba 2011.

Juni 2012 alipigwa kalamu tena pamoja na kamati yote simamizi ya timu hii baada ya Kenya kukosa kufuzu kwea michuano ya Afcon 2013.

Aliingia katika ukufunzi wa timu ya Tusker almaarufu “wanamvinyo” na pia akarejea Mathare United mwaka wa 2015 na baada ya kukaa nje kwa muda, lakini akiwa msaidizi wa kocha Migne, amerejea tena usukani.

“Mimi kwa kawaida huwa siongei mengi bali napenda kusikiza yanayosemwa. Kwa sasa nimerejea lakini nitangoja kwanza yasemwe na baadaye nitaongea kuhusu Harambee Stars kwa kina,” anasema akiongeza kuwa rekodi yake i wazi kuwa “mimi ni mtu wa matokeo bali sio domo.”

Lakini ameahidi kuwa akiwa na ushirikiano mwema na wadau atatambisha Harambee Stars na ambapo naibu kocha wake atakuwa ni Zedekiah ‘Zico’ Otieno.

Aliingia katika kazi ya ukufunzi wa Harambee Stars kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 32 na kuingia katika rekodi za makocha asili mwenye umri mdogo zaidi nchini kusimamia Kenya.

Anasema kuwa kufaulu katika kazi hii hakuna njia za mkato bali ni “kujituma na kuwa na uzalendo.”

Anasema kuwa ni lazima kuwe na uwiano kati ya wachezaji na kamati ya ukufunzi sambamba na wadau wengine kama serikali na shirikisho la kandanda nchini.

“Utafiti pia. Ni lazima uwe ukijipa ufahamu wa mageni katika safu hii ya ukufunzi na masharti ugani ndio uwajibikie majukumu yako kama kocha vilivyo,” anasema.

Akikiri kuwa nje ya uga anapenda kusoma, kusikiza muziki wa rhumba, akikiri kuwa sekta ya burudani huipenda tu, anasema kuwa anajua “Wakenya wapenzi wa soka wana matarajio mengi kutoka kwangu na Harambee Stars na nitajaribu kadiri ya uwezo wangu kuwapa tabasamu.”

Anasema kuwa kiburi chake ni kuwa “niko katika taifa ambalo linathamini mchezo wa soka na ambapo kuna talanta katika kila pembe ya nchi.”

Anasema kuwa atahakikisha kuwa ameleta usawa katika timu na uwazi wa uteuzi wa timu ya kuwakilisha taifa huku akishirikiana na wengine kusaka vipawa faafu zaidi katika majukwaa ya soka nchini.