Michezo

Harambee Stars kufanyia mazoezi Ufaransa wakifuzu AFCON

October 16th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa Shirikisho la soka nchini(FKF) Nick Mwendwa amefichua kuwa kikosi cha timu ya Taifa, Harambee Stars kitakita kambi ya mazoezi nchini Ufaransa iwapo kitafuzu kushiriki kipute cha Kombe la Bara Afrika mwaka wa 2019 nchini Cameroon.

Harambee Stars wanaongoza kundi F kwa alama saba, alama tatu mbele ya Ethiopia(alama nne) huku Ghana ikivuta mkia kwa alama tatu ingawa wamewajibikia mechi chache ikilinganishwa na wapinzani.

Kocha wa Harambee Stars Sebastien Migne atakuwa na nafasi ya kuandaa kambi ya mazoezi kwa muda wiki mbili katika nchi yake ya asilia ya Ufaransa kabla ya kuelekea Cameroon akilenga kuwatambisha kikosi chake dhidi ya mataifa mengine barani Afrika.

Hata hivyo lazima mkufunzi huyo ahakikishe ametwaa ushindi au sare dhidi ya Ghana au Sierra Leone katika mechi mbili zilizosalia ili kujihakikishia nafasi kwenye fainali hizo.

“Tuna mpango wa kuipeleka timu kushiriki mazoezi nchini Ufaransa kabla ya AFCON 2019 nchini Cameroon,” akasema Mwendwa baada ya kushuhudia mechi dhidi ya Ethiopia Jumapili.

Stars watachuana na Siera Leone nyumbani iwapo Shirikisho la soka duniani FIFA itafutilia mbali marufuku ya CAF kwa taifa hilo la Afrika Magharibi lililomarufikishwa kutokana na serikali yake kuingilia maswala ya soka.

Ingawa hivyo, Kenya itafuzu kwa AFCON mwaka 2019 iwapo marufuku hiyo itadumu.