Michezo

Harambee Stars kupiga kambi Ufaransa kujiandaa kwa AFCON

January 9th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amethibitisha kwamba timu ya taifa ya wanaume almaarufu Harambee Stars itapiga kambi ya mazoezi nchini Ufaransa kabla ya Kombe la Afrika (AFCON) 2019.

Akizungumza na Taifa Leo mnamo Januari 8, 2019 baada ya Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) kutangaza Misri itaandaa kindumbwendumwe hicho katikati ya mwaka huu, Mwendwa amesema, “Kambi (ya Harambee Stars nchini Ufaransa) iko.

Tunashughulikia suala hili kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao na tutawarifu mengi zaidi baada ya mipango kukamilika.”

Kambi ya Stars nchini Ufaransa ilikuwa kwenye mizani ikitegemea mwenyeji wa AFCON 2019. Katika kikao cha awali na wanahabari, Mwendwa alifichua kwamba Kenya ingeondoa kambi yake kutoka Ufaransa kama dimba la AFCON lingepelekwa Afrika Kusini kutokana na tofauti ya majira ya mwaka.

“Ufaransa itakuwa na majira ya joto kabla ya AFCON kwa hivyo dimba hili likienda katika taifa litakalokuwa na majira ya baridi haitakuwa busara kupelekea Harambee Stars huko.

Itatufaa tu kuenda Ufaransa ikiwa taifa litakalochaguliwa kuandaa AFCON litakuwa na majira yanayopatikana katka nchini itakayopata haki za uenyeji,” alisema baada ya Cameroon kupokonywa uenyeji wa makala haya ya 32.

Kenya ilifuzu kutoka Kundi F baada ya kupepeta Ghana 1-0 Septemba na Ethiopia 3-0 Oktoba jijini Nairobi na kutoka sare dhidi ya Ethiopia ugenini Oktoba.

Itamenyana na Ghana ugenini katika mechi ya marudiano mwezi Machi, mechi ambayo pia itaamua mshindi wa kundi hili.

Ghana pia ilifuzu baada ya kulipua Ethiopia 5-0 mjini Kumasi na kuilima 2-0 katika mechi ijayo nchini Ethiopia. Ethiopia ilisalia na alama moja baada ya Sierra Leone kupigwa marufuku na Shirikiso la Soka Duniani (FIFA) mnamo Oktoba 5, 2018 serikali ilipoingilia shughuli za shirikisho la soka nchini humu kufuatia madai ya ufisadi.