Harambee Stars kupimana nguvu dhidi ya Sudan Kusini na Tanzania kabla ya kibarua cha Misri

Harambee Stars kupimana nguvu dhidi ya Sudan Kusini na Tanzania kabla ya kibarua cha Misri

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya wanaume ya Kenya, Harambee Stars itapimana nguvu dhidi ya majirani Sudan Kusini na Tanzania kabla ya mechi za kufa-kupona za kuingia Kombe la Bara Afrika (AFCON).

Kenya, ambayo imeratibiwa kuanza mazoezi mnamo Februari 29, itaalika Bright Stars Sudan Kusini mnamo Machi 13 halafu ikabane koo na Taifa Stars ya Tanzania mnamo Machi 15 na Machi 18. Michuano hiyo yote ya kupimana nguvu itasakatwa nchini Kenya. Uwanja/viwanja vitakavyotumiwa bado havijatangazwa, ingawa uwanja wa kitaifa wa Nyayo na ule wa kimataifa wa Kasarani vimetumika hivi majuzi kwa mechi za kimataifa.

Kenya, ambayo inakamata nafasi ya 104 katika viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani, inanolewa na Jacob ‘Ghost’ Mulee. Katika kampeni za kuingia AFCON2022, Kenya iko katika Kundi G pamoja na miamba Misri, wanavisiwa wa Comoros na Togo kutoka Magharibi mwa Afrika.

Nambari 135 duniani Tanzania inapatikana katika Kundi J pamoja na Tunisia, Equatorial Guinea na Libya.

Sudan Kusini, ambayo tayari imetangaza itawasili Kenya mnamo Machi 9, ni ya 163 duniani. Iko katika Kundi B ambalo pia linajumuisha Burkina Faso, Uganda na Malawi.

Kenya inahitaji ushindi pekee dhidi ya Mafirauni wa Misri na Sparrowhawks ya Togo na kuomba mmoja kati ya Misri na Comoros apoteze michuano yake yote iliyosalia ili iingie AFCON2022 nchini Cameroon.

Vijana wa Ghost Mulee wameshinda Tanzania mara mbili mfululizo pia Sudan Kusini kwa hivyo wataanza michuano hiyo ya kirafiki na rekodi nzuri, ingawa wachezaji wake wengi kutoka ligi za kigeni huenda hawatakuwa wamefika kucheza dhidi ya Bright Stars na mechi ya Tanzania ya kwanza. Bright Stars inanolewa na mzawa wa Ujerumani mwenye asili ya Cameroon Cyprian Besong Ashu nayo Tanzania iko chini ya raia wa Burundi Etienne Ndayiragije.

You can share this post!

Madaraka Scarlets yawakilisha Freearea soka ya akina dada

Dkt Ahmed Kalebi awapa motisha Gogo Boys kujitahidi zaidi...