Michezo

Harambee Stars kupimana nguvu na Malawi Kasarani

September 2nd, 2018 2 min read

Na Geoffrey Anene

Harambee Stars ya Kenya itapimana nguvu na The Flames ya Malawi katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi mnamo Septemba 10 ama Septemba 11, 2018.

Tovuti ya michezo ya Soka imenukuu Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa akisema, “Ni kweli tutakuwa wenyeji wa Malawi hapo Septemba 10 katika mechi ya kirafiki.”

Naye Katibu wa Shirikisho la Soka la Malawi (FAM) Alfred Gunda ameeleza gazeti la Nyasa Times nchini humo kwamba timu hizi zitamenyana Septemba 11.

Kenya inajiandaa kupepetana na Ghana katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) ya Kundi F uwanjani Kasarani hapo Septemba 8. Vijana wa kocha Sebastien Migne hawana pointi baada ya kufungua kampeni yao kwa kulazwa 2-1 na Sierra Leone jijini Freetown mwaka 2017. Ghana inaongoza kwa alama tatu baada ya kuaibisha Ethiopia 5-0 mjini Kumasi.

Malawi pia itakuwa ikitafuta tiketi ya kuingia AFCON mnamo Septemba 8 itakapokabiliana na Morocco katika mechi ya Kundi B mjini Rabat. The Flames, ambayo Nyasa Times imeripoti itaelekea nchini Morocco hapo Septemba 5, ilianza kampeni yake kwa kubwaga wanavisiwa wa Comoro 1-0 jijini Blantyre. Inashikilia uongozi wa kundi hilo kwa pamoja na mabingwa watetezi Cameroon, ambao walinyamazisha Morocco 1-0 jijini Yaounde.

Kenya na Malawi zitatumia mchuano huu wa kirafiki kujipiga msasa kabla ya mechi mbili muhimu mwezi Oktoba. Vijana wa Migne wataelekea Ethiopia mnamo Oktoba 10 kabla ya majirani hawa kurudiana Oktoba 13 jijini Nairobi. Malawi itakuwa nchini Cameroon mnamo Oktoba 10 na kualika miamba hao nchini Malawi siku tatu baadaye.

Kenya na Malawi ziliumiza nyasi bure zilipokutana mara ya mwisho Aprili mwaka 2017 katika mechi ya kirafiki uwanjani Kenyatta mjini Machakos.

Harambee Stars itaanza mazoezi uwanjani Utalii mtaania Ruaraka mnamo Septemba 2. Wachezaji wa kimataifa akiwemo nahodha Victor Wanyama kutoka Tottenham Hotspur nchini Uingereza, wanatarajiwa kuanza kuwasili nchini Septemba 2 jioni.

Kikosi cha Kenya: David Owino, Jesse Were, Anthony Akumu (Zesco United, Zambia), David Ochieng’, Eric Johanna (Brommapojkarna, Uswidi), Erick Ouma, Ovella Ochieng (Vasalund, Uswidi), Johanna Omollo na Abud Omar (Cercle Brugge, Uswidi), Ian Otieno (Red Arrows, Zambia), Ismael Gonzalez (Fuenlabrada, Uhispania), Clifton Miheso (Buildcon, Zambia), Musa Mohammed (Nkana, Zambia), Joseph Okumu (Ann Arbor, Marekani), McDonald Mariga (Real Oviedo, Uhispania), Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan), Paul Were (Kaisar, Kazakhstan), Brian Mandela (Maritzburg United, Afrika Kusini), Victor Wanyama (Tottenham Hotspur, Uingereza), Boniface Oluoch, Philemon Otieno, Joash Onyango, Francis Kahata, George Odhiambo, Samuel Onyango (wote Gor Mahia), Dennis Odhiambo, Piston Mutamba (wote Sofapaka), Whyvonne Isuza, Duncan Otieno (wote AFC Leopards), Farouk Shikalo, Abdallah Hassan (wote Bandari), Brian Bwire (Kariobangi Sharks), Jockins Atudo (Posta Rangers), Benard Ochieng’ (Vihiga United), Cliff Nyakeya (Mathare United), Allan Wanga (Kakamega Homeboyz), Masud Juma (hana klabu) na Patrick Matasi (Tusker).