Michezo

Harambee Stars ugani Paris dhidi ya Madagascar

June 7th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

KOCHA Sebastien Migne wa Harambee Stars leo Ijumaa ataongoza vijana wake nchini Ufaransa kukabiliana na Madagascar katika mechi ya kupimana nguvu.

Mechi hiyo ya kwanza katika maandalizi ya vijana hao wanaojiandaa kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) itachezewa katika uwanja wa French Rugby Federation Complex jijini Paris, Ufaransa ambako kikosi hicho kimepiga kambi kwa mazoezi ya wiki tatu kabla ya kuelekea Misri.

Huenda Migne akaunga kikosi chake bila mshambuliaji matata Michael Olunga ambaye alikuwa hajafika kambini kufikia Jumatano.

Katika michuano ya AFCON, Harambee Stars imepangwa katika Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Tanzania.

Nayo Madgascar nao wamepangwa pamoja na Nigeria, Guinea na Burundi katika Kundi B ambapo wamepangiwa kuanza dhidi ya Guinea mnamo Juni 22.

Madagascar chini ya Nicolas Dupuis ilitoka sare 3-3 na Luxemburg katika mechi nyingine ya kujipima nguvu, Jumapili.

Luxemburg inaorodheshwa ya 86 kwenye viwango vya kimataifa vya FIFA huku Madagascar wakiwa katika nafasi ya 107.

Kocha Dupuis anatarajiwa kuteremsha uwanjani kikosi kilichocheza Jumapili huku akiwategemea Pauli Voavy, Faneva Andriastsima na Charles Andriamanitsinoro kuongoza mashambulizi.

“Naifahamu Kenya kama timu inayocheza mchezo wa kutumia nguvu, lakini wasitarajie mteremko. Wengi wametupuuza kwa vile hii ndio mara yetu ya kwanza kufuzu kwa AFCON, lakini tutawashangaza wengi vile vile,” alisema kocha Dupuis.

“Tumejiandaa vyema kukabiliana na upinzani wowote. Tulikubali kucheza na Kenya kwa vile kundini pia tuko na timu zinazocheza kama wao. Harambee Stars wanajivunia wachezaji wengi wenye nguvu, huku wingi zao zikiwa matata, mbali na ukuta imara wa kulinda ngome,” alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 51.

Wakati huo huo, mshambuliaji Masoud Juma ambaye awali alikuwa nyota wa Kariobangi Sharks amepuuza wanaoendelea kulalamika kufuatia kuingizwa kwake kikosini huku akidai atawafurahisha mashabiki hao wasiomuamini.

“Nilipokuwa na SoNy Sugar na kuitwa katika kikosi cha Harambee Stars, wengi walifurahia, na pia nilipokuwa na Bandari na nikapata muaaliko huo, walifurahia, lakini ni wakati huu tu wamekasirika kwa vile sikuwa nikichezea hapa nchini. Nimekuwa nikisakata nchini Libya, lakini kutokana na hali mbaya ya kisiasa nchini humo, singeweza kuvuma zaidi,'” aliongeza.

Wakenya wengi walimfokea kocha Migne kwa kumjumuisha Masoud badala ya Jesse Were wa Zesco United wala Allan Wanga wa kakamega Homeboyz.

Mbali na Masoud, washambuliaji wengine kikosini humo ni Ovella Ochieng wa Kariobangi Sharks na John Avire wa Sofapaka.