Michezo

Harambee Stars warejea nchini mikono mitupu

June 12th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Sebastien Migne na vijana wake wa Harambee Stars wamerejea nchini mikono mitupu kutoka India.

Stars ilialikwa kushindania taji la Hero Intercontinental Cup mjini Mumbai na kumaliza katika nafasi ya pili.

Ilinyamazishwa 2-0 na wenyeji India katika fainali iliyosakatwa Juni 10. Mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) walilima New Zealand 2-1, wakachapwa 3-0 na India katika mechi ya pili kabla ya kutinga fainali baada ya kulipua Chinese Taipei 4-0.

Vijana wa Migne walialikwa dakika ya mwisho kushiriki mashindano hayo ya mataifa manne baada ya Afrika Kusini kujiondoa.

Walitumia mechi hizo kujipima nguvu kabla ya kurejelea kampeni ya kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019.

Kenya iko katika Kundi F pamoja na Ghana, Sierra Leone na majirani Ethiopia.

Ilianza kampeni kwa kulazwa 2-1 na Sierra Leone jijini Freetown mwezi Juni mwaka 2017. Mechi yake ya pili ni dhidi ya Ghana mwezi Septemba nchini Kenya kabla ya kusafiri Ethiopia mnamo Oktoba 10 na kisha kualika Waethiopia nchini Kenya mnamo Oktoba 13.

Wakenya watafunga mwaka 2018 kwa kukaribisha Sierra Leone humu nchini mwezi Novemba. Kenya itazuru Ghana mwezi Machi mwaka 2019 kwa mechi yake ya mwisho.

Matokeo ya Kenya (Hero Continental Cup):

Mechi za raundi ya kwanza

Kenya 2-1 New Zealand (Juni 2, 2018)

Kenya 0-3 India (Juni 4, 2018)

Kenya 4-0 Chinese Taipei (Juni 8, 2018)

Fainali

India 2-0 Kenya (Juni 10, 2018)