Michezo

Harambee Stars yabadili kipa sababu ya jeraha Cecafa ikinukia

December 3rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Francis Kimanzi amefanyia idara ya unyakaji wa mipira ya timu ya taifa ya Harambee Stars badiliko la lazima baada ya kipa Brian Bwire kujiondoa kwa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenge Cup) kutokana na jeraha la kinena.

Nafasi ya nyota huyo wa timu ya Kenya ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 na klabu ya Katiobangi Sharks, imejazwa na kipa wa Western Stima, Samuel Odhiambo.

Kimanzi pia ameongeza mshambuliaji Timothy Otieno (Tusker FC) na kiungo Mohammed Katana (Bandari FC) katika kikosi cha wachezaji 26 alichotaja Novemba 30. Kenya, ambayo ilishinda makala yaliyopita mwaka 2017 mjini Machakos, italimana na Tanzania, Djibouti na Zanzibar katika mechi za Kundi C katika makala ya mwaka huu yatakayofanyika nchini Uganda kutoka Desemba 7-19.

Vijana wa Kimanzi waliratibiwa kuanza mazoezi hapo jana.

Kundi A linajumuisha wenyeji Uganda pamoja na Burundi, Ethiopia na Eritrea, huku Kundi B likikutanisha wageni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Sudan, Sudan Kusini na Somalia.

Timu mbili za kwanza kutoka makundi yote matatu pamoja na timu mbili zitakazomaliza mechi za makundi katika nafasi ya tatu zikiwa na alama nyingi zitaingia robo-fainali.