Michezo

Harambee Stars yamiminiwa sifa kwa sare na UG

September 10th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WIKI tatu baada ya uteuzi wa Francis Kimanzi kuongoza timu ya taifa ya soka ya Kenya almaarufu Harambee Stars kuonekana kugawanya Wakenya, mashabiki mnamo Jumapili walikuwa wakiimba wimbo mmoja wakimmiminia sifa kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Uganda.

Majirani hao walikabana koo katika mechi safi ya kirafiki uwanjani Kasarani mnamo Septemba 8, ambayo Mganda Emmanuel Okwi alipeleka timu yake mapumzikoni ikiwa kifua mbele kabla ya Kenneth Muguna kusawazishia wenyeji katika kipindi cha pili.

Mashabiki wengi wanasema sare ni mwanzo mwema kwa Kimanzi, ingawa wamemtaka Stars kuimarika katika mechi zijazo.

Shabiki GK Freddy alisema, “Leo, tulisakata mechi ya kuvutia. Hongera timu ya Kenya. Tunajivunia kazi yenu.”

Nyamongo Gekara, “Tunahitaji kumuamini Kimanzi. Anaweza kurejesha Stars katika nafasi ya 68 duniani. Tutakuwa katika Kombe la Afrika (Afcon) na mara hii, tutafanya vyema zaidi.”

Lawrence Kivindu Mutua, “Nimeshuhudia ushirikiano mwema kutoka kwa Stars, pongezi vijana wetu, benchi la kiufundi na viongozi bila kuwasahau mashabiki.”

Mmoja wa mashabiki hao, Lusher Paulo alidai, “Kimanzi kuanza na sare ya 1-1 dhidi ya Uganda ni mwanzo mzuri kwa sababu kucheza na Uganda ni sawa na kumenyana na Misri. Uganda si timu rahisi.”

 

Michael Olunga wa Harambee Stars akabiliwa na Timothy Awany wa Uganda Cranes (chini) wakati wa mchuano wa kirafiki uliowakutanisha uwanjani Kasarani. Picha/ Chris Omollo

Naye Jacktoh Abedi, “Timu iko sawa. Natumai itadumisha mchezo wake na kivyangu, nadhani Kimanzi atatufikisha mbali.”

Peterson Kirimi, “Kipindi cha pili kilikuwa safi kwetu. Wachezaji wa akiba ambao Kimanzi alitumia walidhihirisha kuwa kocha huyu anafahamu wachezaji wake.”

Mashabiki pia walimpendekezea Kimanzi vitu kadhaa wanavyoamini vitaimarisha timu. Peter Kabugy Mwangi, “Ilikuwa mechi safi, ingawa inafaa tupate suluhu ya safu ya kati. (Michael) Olunga anafaa kupata wachezaji wazuri katika idara hiyo ndiposa aweze kukamilisha weledi wake wa kufunga mabao!”

Kev de Prince, “Kazi safi, lakini tunahitaji mshambuliaji mwingine mzuri kusaidiana na Olunga, ambaye alikuwa amekabwa sana. Ingawa tuliamka katika kipindi cha pili, Kimanzi anastahili kuimarisha safu yetu ya kati na kutafuta njia ya kutia makali katika ushambuliaji. Pia, tunahitaji beki mzuri wa pembeni kulia.”

Naye Johnte Chombar alikuwa na ujumbe kwa Shirikisho la Soka nchini (FKF) akisema, “Hatutahiji kocha wa kigeni. Lazima tusaidie kocha wa hapa nchini.” Aidha, mashabiki wengine walilaumu FKF kwa kutopeperusha mechi hiyo na kuitaka ihakikishe mechi za Stars zijazo zinaonyeshwa katika runinga ya kitaifa.

Stars ilitumia mechi hiyo kujipima nguvu kama sehemu ya maandalizi yake ya mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2021. Vijana wa Kimanzi watapepetana na Libya na Msumbiji katika mechi zingine za kirafiki.

Watachapana na Misri, Togo na Comoros katika mechi za Kundi G za kufuzu kushiriki makala yajayo ya Afcon.