Harambee Stars yapiga Togo 2-1 bila Olunga

Harambee Stars yapiga Togo 2-1 bila Olunga

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya soka ya Kenya maarufu kama Harambee Stars ilibanduka kwenye michuano ya kuingia Kombe la Afrika (AFCON) 2022 kwa heshima baada ya kuchapa Togo 2-1 jijini Lome hapo Jumatatu.

Katika mechi hiyo yao ya mwisho ya Kundi G, ambayo kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee alikosa huduma za mshambuliaji wa Al Duhail, Michael Olunga maarufu kama Engineer, beki Joash “Berlin Wall” Onyango, kipa nambari moja Ian Otieno na kiungo Lawrence Juma baada ya wachezaji hao kupatikana na virusi vya corona, Kenya ilitinga bao katika kila kipindi.

Mshambuliaji wa Bandari FC Abdalla Hassan alitikisa nyavu dakika ya 32 baada ya kumegewa pasi murwa kutoka winga wa Gor Mahia, Cliffton Miheso.

Bao hilo ni la tatu katika mechi tatu ambazo Hassan amesakata baada ya kuona lango Kenya ikibwaga Tanzania 2-1 ugani Nyayo katika mechi ya kirafiki Machi 18 na pia katika sare ya 1-1 dhidi ya Mafirauni wa Misri mnamo Machi 25 katika mechi ya kuingia AFCON2022.

Mshambuliaji wa zamani wa Bandari, Masud Juma, ambaye ni mali ya Difaa Hassani El Jadidi nchini Morocco, aliongeza bao la pili dakika ya 63 kupitia penalti. Hii ilikuwa ni dakika mbili tu baada ya Mulee kupumzisha Nahashon Alembi na kujaza nafasi yake na Harun Mwale.

Miheso alipumzishwa dakika ya 72 na nafasi yake kutwaliwa na Kevin Simiyu. Togo ilipata bao la kufuta machozi dakika ya tatu ya majeruhi kupitia penalti kutoka kwa Henri Eninful.

Misri ilikamilisha juu ya kundi hili kwa alama 12 kutokana na ushindi mara tatu ikiwemo kulipua Comoros 4-0 Machi 29 na sare tatu.

Comoros, ambayo itashiriki AFCON kwa mara ya kwanza kabisa katika historia yake, ilimaliza kampeni yake katika nafasi ya pili kwa alama tisa. Kenya ilizoa alama saba kutokana na ushindi huo wake wa kwanza na, sare nne na kichapo kimoja.

Togo ilikamilisha mkiani mwa kundi kwa alama mbili. 

You can share this post!

Mshtuko huku corona ikiua maafisa 5 wa kaunti

IEBC yaidhinisha wawaniaji 6 wa ubunge Juja